Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CR7, hadithi yake inasikitisha lakini ameandika mwenyewe

PAZIA Pict


WAKATI mwingine waandishi wazuri wa hadithi za mapenzi huwa wanashindwa kumalizia simulizi nzuri za hadithi za mapenzi wanazoandika. Au labda ndivyo ambavyo hadithi huwa inasisimua zaidi? Labda.


Kwa mfano ilivyotokea katika hadithi ya Diego Maradona. Yeye na mpira walipendana. Moja kati ya vipaji vya ajabu vilivyowahi kutokea katika mpira. Kwa kutumia mguu wake wa kushoto peke yake aliwaongoza Waargentina kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1986.


Pamoja na kila kitu, Maradona alikuwa anatumia dawa za kulevya huku akiwa na matukio mengi ya ajabu ndani na nje ya uwanja. Katika upande huu ina maana mwandishi asingeweza kuandika hadithi yake vizuri. Kuna maisha ya mastaa wengi ndani ya nje ya soka ambayo hayakukamilika vizuri.

PAZ 01

Kuna Mike Tyson ambaye ambaye hakuna na mfano wake katika ngumi za uzito wa juu (heavyweight), lakini nje ya ulingo wa ngumi alikuwa na matukio mengi. Aliwahi kwenda jela, aliwahi kufilisika, aliwahi kukumbwa na kila baya ambalo lisingemfanya mwandishi wa hadithi ya maisha yake awe ameandika kitabu kikamilifu cha maisha yake.

Kuna simulizi nyingi. Mfano mwingine ni huu hapa. Huu hapa wa Cristiano Ronaldo. Mmoja kati ya wanasoka bora kuwahi kutokea ulimwenguni. Bora kabisa. Rekodi yake ya mabao inatisha. Amefunga mabao mengi nyuma ya Pele.

Hata hivyo, Jumatatu mchana Ronaldo aliondoka katika Uwanja wa Arlington pale Dallas akihitimisha maisha yake ya soka bila ya kutwaa kombe la dunia. Mwandishi wa simulizi yake ya mapenzi kati ya yeye na mpira aliondoa kipande hiki cha Ronaldo kutwaa kombe la dunia.

PAZ 02

Unaweza kudai kwamba hata Neymar amestaafu kuichezea timu ya taifa ya Brazil bila ya kutwaa kombe la dunia. Sikiza. Ronaldo ni mkubwa sana kuliko Neymar. Ronaldo huwa anawekwa katika Kundi la hasimu wake, Lionel Messi, Pele, Maradona, Ronaldinho, Ronaldo di Lima na wachezaji wa namna hii.

Ronaldo ametua katika uwanja wa ndege wa Lisbon bila ya taji. Umri ni miaka 41 na miaka minne ijayo kombe la dunia litafanyika pia katika ardhi ya kwao Ureno. Hii ina maana gani? Atakuwa na umri wa miaka 45. Hakuna mchezaji aliyewahi kucheza kombe la dunia akiwa na umri huo.

Hata umri huu aliokwenda nao katika kombe la dunia yeye mwenyewe anaweza kuwa sababu ya Ureno kutofika mbali au kutwaa taji lenyewe. Ronaldo ana ubinafsi. Ana jina kubwa ambalo limemtisha kocha wake, Roberto Martinez.

PAZ 03

Unapozingatia kwamba tabia zake binafsi ni za kibinafsi zaidi na ana njaa kali ya kucheza, Martinez hakuwa na jinsi zaidi ya kufuata lugha ya mwili ya Ronaldo. Makocha wengi huwa wanatishika na Ronaldo.

Ni wachache ambao walijaribu kiburi kwake. Mmojawapo ni Erik Ten Hag pale Old Trafford. Ronaldo alikuwa hataki kutolewa uwanjani. Alikuwa hataki kuanzia benchi. Ten Hag ndiye kocha wa kawaida ambaye alichukua maamuzi yake binafsi dhidi ya Ronaldo bila ya kumjali Ronaldo.

Martinez alikuwa tayari kuona jahazi linazama kwa ajili ya kumbeba Ronaldo. Aliacha damu changa nyingi katika benchi lakini kwanza kabisa hakuweza kumuweka benchi Ronaldo na pili alikuwa anahofia kumtoa.

PAZ 04

Miguu ya Ronaldo ilikuwa imechoka na kuna wakati alionekana kichekesho uwanjani. Ureno ilihitaji makocha wakubwa kwa ajili ya kumpiga benchi Ronaldo au kutomuita kabisa katika kikosi. Makocha kama Pep Guardiola na Jose Mourinho angeweza kufanya hivyo.

Kuna baadhi ya mashabiki wameanza lawama kwa viungo wa Ureno kama Bruno Fernandes kwamba walikuwa hawampi pasi Ronaldo. Ukweli ni kwamba unampaje pasi mchezaji ambaye hafungui nafasi mara kwa mara?

Kwa Ronaldo mwenyewe, kama asingekuwa mbinafsi vijana wangeweza kumpambanoia ndoto yake ya kutwaa kombe la dunia. Angeweza kuamua kucheza dakika chache za mwisho wakati wapinzani wakiwa wamechoka.

PAZ 05

Mwisho wa siku kama Ureno ingetwaa kombe la dunia bado angeingia katika orodha ya wachezaji waliotwaa kombe la dunia. Hata hivyo bado alijiona ana nguvu ya kuisaidia Ureno kutwaa kombe la dunia akiwa ndani ya uwanja, tena huku akicheza dakika zote.

Mpaka tunapozungumza Ronaldo hajatangaza kustaafu timu ya taifa ya Ureno ingawa amekiri kwamba hii itakuwa michuano yake ya mwisho ya kombe la dunia. Kinachoonekana ni kwamba anailenga michuano ya Euro 2028.

Kocha mpya wa Ureno ni Jorge Jesus. Kinachochekesha ni kwamba alikuwa kocha wa Ronaldo na Joao Felix katika kikosi cha Al Nassr. Kule alikuwa analazimika kumpanga Ronaldo kwa muda wote kwa sababu inasemekana Ronaldo ana mkataba maalumu wa kucheza kila mechi kwa kadri anavyojisikia.

PAZ 06

Nataka kuona kama Jesus ataendelea kuwekwa mfukoni na Ronaldo katika kikosi cha Ureno. Anahitajika kuwa na maamuzi magumu kwa ajili ya kulinda kibarua chake vinginevyo anaweza kuingia katika mkumbo wa Martinez wa kupotezewa kibarua na Ronaldo.

Mwisho wa siku pamoja na kila kitu bado naamini kitu ambacho nimekuwa nikikiamini siku zote. Kwamba kutwaa kombe la dunia sio kigezo cha mchezaji kuitwa mchezaji bora wa muda wote. Najaribu kufikiria tu kwamba kama ambavyo imetokea kwa Ronaldo ingeweza kutokea kwa Messi.

Hauwezi kusema Ronaldo sio mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote kwa sababu tu hajatwaa kombe la dunia. Sio kweli. Nawafahamu wachezaji wengi wa kawaida ambao wametwaa kombe la dunia kama ambavyo nawafahamu wachezaji wengi mahiri kando ya Ronaldo ambao hawajawahi kutwaa kombe la dunia.