Bao la Simchimba kuchunguzwa upya na Bodi ya Ligi

Muktasari:
- Nyota huyo ana mabao 19, ingawa katika kumbukumbu za TPLB ameandikiwa 18, kwa kile kilichotokea katika mchezo huo dhidi ya Cosmopolitan uliopigwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani, ambao kikosi hicho kiliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
UTATA wa bao moja alilonyimwa mshambuliaji wa Geita Gold, Andrew Simchimba limetua kwa Bodi ya Ligi (TPLB) na kwa sasa wanafanya uchunguzi kwa kilichotokea katika mchezo wa Championship dhidi ya Cosmopolitan, Novemba 24, 2024.
Nyota huyo ana mabao 19, ingawa katika kumbukumbu za TPLB ameandikiwa 18, kwa kile kilichotokea katika mchezo huo dhidi ya Cosmopolitan uliopigwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani, ambao kikosi hicho kiliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo ndio ilioleta utata zaidi wa kunyimwa bao, ikielezwa Kamishna aliandika kimakosa aliyefunga mabao yote kwa upande wa kikosi cha Geita Gold alikuwa ni Frank Ikobela, japo nyota huyo na Simchimba kila mmoja wao alifunga moja.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda alisema wataangalia upya ripoti ya mechi hiyo na wakijiridhisha nyota huyo atapewa bao lake, kwani wao kama mamlaka hawana nia mbaya ya kumnyima mtu haki yake.
“Kama ripoti iliyoletwa iliandikwa kimakosa huwa tunairekebisha kwa sababu ni mambo ya kawaida, hatuko tayari kumnyima mtu haki yake, tutaipitia tena upya na ikigundulika tutamuongezea bao lake moja na wala hilo halina tatizo,” alisema Boimanda.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Geita Gold, Samwel Dida alisema licha ya wote waliofunga mabao hayo ni wachezaji wa timu hiyo, ila ni vyema haki ikatendeka, kwani wanataka kuona Simchimba anaibuka kidedea na tuzo ya mfungaji bora msimu huu.
Kwa upande wa Simchimba, alisema anaamini haki itatendeka na ataongezewa bao lake moja, ili kuondoa utata mwishoni mwa msimu huu, ikiwa zaidi ya wachezaji wawili watashikana kwa idadi sawa ya mabao kama hali itaendelea ilivyokuwa kwa sasa.
Simchimba ikiwa ataongezewa bao hilo atafikisha mabao 19 tofauti na ilivyokuwa sasa anavyoandikwa na 18, nyuma ya nyota wa TMA, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ mwenye 17, akifuatiwa na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh aliyefunga 16.