Baleke, Simba na Yanga kuna kitu, ataja aliyemleta Dar

Muktasari:

  • Baleke alijiunga na Al-Ittihad, akitokea Simba ambapo kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam na tetesi za kuhitajika na hizo klabu zimekuwa kubwa.

SIMBA na Yanga, zinaweza zikaingia vitani kuwania saini ya straika Jean Baleke wa Al-Ittihad ya Libya, baada ya kuwepo na taarifa kufuatwa na viongozi wa klabu hizo.

Baleke alijiunga na Al-Ittihad, akitokea Simba ambapo kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam na tetesi za kuhitajika na hizo klabu zimekuwa kubwa.

Mwanaspoti, lilionana na Baleke jana, ili kufafanua kuhusiana na taarifa za kutafutwa na klabu hizo na kama ndiyo sababu ya ujio wake jijini Dar es Salaam.

“Kwanza nipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mambo yangu, hapa ni kama nyumbani, kwani hakuna mambo ya viza kati ya Tanzania na Congo, hivyo naweza kuja wakati wowote na Watanzania wanaweza kwenda Congo wakati wowote,” alisema na kuongeza;

“Nilisaini Al-Ittihad kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, nimetumikia miezi sita, imesalia sita, endapo kama kuna timu ambayo inanihitaji, ije tuzungumze, kazi yangu ni mpira kikubwa ni makubaliano kwenye maslahi.

“Kuhusu Simba ni kama nyumbani, naweza kurudi kuichezea endapo kama watanihitaji, ingawa maslahi yatapanda kidogo, kulingana na ninacholipwa Al-Ittihad.”

Anaulizwa vipi kuhusu Yanga? Anajibu; “Sijapata ofa rasmi, naona mitandaoni na wakati wa mkutano wa Yanga, watu walinipigia sana simu, wakidhani nakwenda kutambulishwa huko, hapana sijasaini Yanga.”

Ukiachana na hilo, Baleke alisema bado ana mkataba na TP Mazembe, hivyo kama kuna timu yoyote ambayo, itakuwa inahitaji huduma yake, itatakiwa kwenda kuzungumza na waajiri wake.

“Nimebakiza mkataba wa mwaka mmoja na TP Mazembe, timu ambazo zinanitaka,zitazungumza na viongozi wangu,” alisema.

Baleke ndiye mfungaji bora wa mabao 14, akiwa na hat-trick nne, alicheza mechi nane katika ligi ya Libya. 

Alijiunga Simba usajili wa dirisha dogo la msimu 2022/23 alimaliza na mabao manane na msimu ulioisha alioachwa dirisha dogo na kuibua maswali mengi kwa mashabiki.