Baba Sure Boy auweka mpira kati Kariakoo Dabi

Muktasari:

  • Mkongwe huyo aliyewahi kuichezea Yanga SC, amesema kwenye makaratasi Yanga imeonyesha kiwango cha juu kwenye mechi mbalimbali, lakini hilo halitoshi kuona ni rahisi kuikabili Simba.

Abubakar Salum 'Sure Boy Sr' ambaye ni baba mzazi wa kiungo wa Yanga, Salum Abubakar 'Sure Boy', amesema Kariakoo Dabi haijawahi kutabirika, haijalishi ni timu gani inakuwa kwenye kiwango kizuri kwa wakati huo.

Mkongwe huyo aliyewahi kuichezea Yanga SC, amesema kwenye makaratasi Yanga imeonyesha kiwango cha juu kwenye mechi mbalimbali, lakini hilo halitoshi kuona ni rahisi kuikabili Simba.

"Dakika 90 zina maajabu na zina nguvu zaidi kwenye mchezo wa dabi, ingawa nikiitazama Yanga naipa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, ila natambua utakuwa mchezo mgumu na ushindani," amesema.

Alipoulizwa endapo kijana wake atacheza Kariakoo Dabi ni ujumbe gani anampa, akasema: "Namtakia kila la kheri timu yake ishinde, akicheza ahakikishe anaacha alama ambayo itakuwa inasimuliwa kwani dabi inampa mchezaji heshima kubwa."

Baba yake Sure Boy aliyekuwa mchezaji wa Yanga na Taifa Stars, amemaliza kwa kusema ana uzoefu na dabi hizo, wachezaji wanapaswa kupambania nembo ya klabu, jambo linaloibua ushindani zaidi.