Baada ya kichapo, Maximo abadili mbinu

Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Mbrazil Marcio Maximo akifuatilia pambano kati ya timu yake na Mtibwa Sugar mjini Morogoro. Picha na Mpigapicha wetu
Muktasari:
Juzi Jumamosi, ikicheza mbele ya umati wa mashabiki wake waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali nchini, Yanga ilianza vibaya Ligi Kuu Bara kwa kuruhusu kipigo kutoka Mtibwa, mabao yakifungwa na Mussa Mgosi na Ame Ally.
KOCHA wa Yanga, Marcio Maximo amekubali kushindwa mbele ya Mtibwa Sugar na kusema mipango yake yote haikufanikiwa hadi akafungwa mabao 2-0 lakini ameapa kufumua baadhi ya mbinu zake ili apate ushindi katika michezo inayofuata.
Juzi Jumamosi, ikicheza mbele ya umati wa mashabiki wake waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali nchini, Yanga ilianza vibaya Ligi Kuu Bara kwa kuruhusu kipigo kutoka Mtibwa, mabao yakifungwa na Mussa Mgosi na Ame Ally.
Yanga ambayo haikuruhusu bao katika mechi tano za mwanzo ilizocheza kabla ya Ligi Kuu, iliyumba baada ya beki wa kushoto Oscar Joshua kuumia na nafasi yake kuchezeshwa Mbuyu Twite na Omega Seme kucheza kiungo. Maximo alisema: “Baada ya mabadiliko hayo tulipotea kidogo, nikajaribu kutoa maelekezo fulani pia haikusaidia japokuwa kuna wakati tulicheza vizuri hakuna anayependa kufungwa.
“Kuna kitu nitakifanya kuhakikisha kikosi kinabadilika na kuiletea timu ushindi katika mechi zinazofuata hakika tutakuwa vizuri lakini niseme tu wapinzani wetu wametumia vizuri nafasi walizopata.”
Maximo alikiri mipango yake kuvurugika baada ya kuumia Joshua na kusema sasa atafanyia kazi kujua nini cha kufanya hali kama hiyo ikitokea tena.
“Alipoumia Oscar (Joshua) ndipo mipango yangu ilipovurugika, nililazimika kufanya mabadiliko ambayo sikuyapanga na ambayo yalilazimu kubadili mfumo wa timu, hili pia lilitugharimu.
“Nitaangalia nini cha kufanya kabla ya mchezo ujao, ni lazima tufanye marekebisho makubwa kwani hatutaki kabisa kupoteza mchezo tena, mashabiki waendelee kutuunga mkono,” alisema Maximo.
Hata hivyo Maximo aligoma kuzungumza chochote kuhusu straika Genilison Santos ‘Jaja’ aliyekosa mkwaju wa penalti katika mchezo huo. Kabla ya kupoteza mchezo wa Jumamosi, Maximo aliiongoza Yanga kuzifunga Chipukizi 1-0, Shangani 2-0, KMKM 2-0 (Zote za Zanzibar), Thika United 1-0 na Azam Fc 3-0. Straika Jaja ndiye aliyefunga mabao mengi katika mechi hizo, alifunga mabao manne.