Aziz KI kukipiga mara ya kwanza Wydad AC

Muktasari:
- Mchezo huo utakuwa maalumu kwa ajili ya maandalizi ya Wydad kuelekea michuano ya Klabu Bingwa ya Fifa ya Dunia itakayopigwa kuanzia Juni 15, mwaka huu.
LEO huenda ikawa siku ya kwanza kumshuhudia nyota wa zamani wa Yanga na Burkina Faso, Stephane Aziz Ki ndani ya kikosi cha Wydad Athletic Club itakapokuwa ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sevilla kutoka Hispania.
Mchezo huo utakuwa maalumu kwa ajili ya maandalizi ya Wydad kuelekea michuano ya Klabu Bingwa ya Fifa ya Dunia itakayopigwa kuanzia Juni 15, mwaka huu.
Macho ya wapenzi wa soka hasa mashabiki wa Yanga yataelekeza kwenye mchezo huo kumuona Azzi Ki kama atapata nafasi ya kucheza na kuonyesha kile kilichofanya Wydad itoe pesa nyingi kumsajili.
Hivi karibuni Aziz KI alitambulishwa na Wydad ambapo Hamisa Mobetto, ambaye ni mkewe alionekana katika picha akiwa nyota huyo wakati akisaini mkataba wa kuichezea timu hiyo, na Hamisa aliandika katika akaunti yake ya Instagram "Mume wangu kipenzi aziz.ki.10 ❤️.
"Hongera kwa hatua hii kubwa ya kusaini mkataba wako mpya na Wydad AC. Kila wakati naona juhudi zako, bidii yako na tamanio lako la kuwa mchezaji bora sio tu Afrika ila duniani. Dua na kujituma kwako ndio msingi wa mafanikio yako siku zote.
"Wewe ni mfano wa uthubutu, uvumilivu, na maono yaliyojaa matumaini. Kila siku unavyoamka, unaamka na njaa ya mafanikio, na hilo linanipa nguvu pia mimi, kama mkeo.
"Kama mkeo, rafiki yako wa karibu, na shabiki wako wa kwanza, dua yangu kila siku ni ufanikiwe zaidi ya ukubwa unaouota kila mara. Endelea kung’ara, endelea kuamini, endelea kusukuma mipaka ya kile kinachowezekana. Najua huu ni mwanzo mpya wa mambo makubwa zaidi. Mimi niko nyuma yako kila hatua, katika kila pambano, kila goli, na kila ndoto unayopigania."