Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aziz KI amuibua beki wa zamani

AZIZ Pict

Muktasari:

  • Aziz KI aliyeitumikia Yanga kwa misimu mitatu tangu aliposajiliwa 2022 kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ameuzwa Wydad Casablanca ya Morocco inayojiandaa fainali za Kombe la Dunia la Klabu 2025 zinazofanyikia Marekani kuanzia Juni 15 hadi Julai 13.

NYOTA wa zamani wa Yanga, Haji Mwinyi Ngwali, ameshindwa kujizuia na kuibuka akiwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu kuondoka kwa kiungo mahiri, Stephane Aziz KI, kwa kusema klabu hiyo bado ina wachezaji bora wanaoweza kuchukua nafasi yake bila kupunguza ubora wa timu.

Aziz KI aliyeitumikia Yanga kwa misimu mitatu tangu aliposajiliwa 2022 kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ameuzwa Wydad Casablanca ya Morocco inayojiandaa fainali za Kombe la Dunia la Klabu 2025 zinazofanyikia Marekani kuanzia Juni 15 hadi Julai 13.

Akizungumza na Mwanaspoti, Haji Mwinyi aliyeitumikia Yanga kama beki wa kushoto na kutwaa nayo mataji mawili ya Ligi Kuu msimu wa 2015-2016 na 2016-2017, alisema kuwa licha ya mchango mkubwa wa Aziz KI tangu alipojiunga na Yanga, klabu hiyo haina sababu ya kuogopa au kujiona dhaifu kwa kuondoka kwa kiungo mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso.

Haji Mwinyi alisema hii ni kwa sababu anaamini kwamba Yanga bado ina hazina kubwa ya vipaji.

“Yanga haiwezi kuwa na pengo la Aziz KI. Ameondoka akiwa ameacha alama kubwa, lakini wapo wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kuvaa viatu vyake,” alisema Mwinyi.

Kwa mujibu wa Mwinyi, wachezaji wanaoweza kurithi jukumu la Aziz KI kikosini hapo kwa sasa ni Pacome Zouzoua na Clatous Chama, akiwachambua kuwa, wawili hao wamewahi kuonesha kiwango cha juu katika mechi muhimu na wana uzoefu wa kutosha wa michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

“Zouzoua ana uelewa mzuri wa mpira, anapiga pasi za mwisho kwa akili na ana uwezo wa kufunga. Chama naye tumemwona mara nyingi akiwa Simba, ni mchezaji wa mechi kubwa. Sasa akiwa Yanga, atakuwa na nafasi ya kuonesha makali zaidi,” alisema beki huyo wa zamani wa KMKM.

Zouzoua ambaye amekuwa akishambulia akitokea pembeni, msimu huu amefunga mabao tisa na kutoa asisti nane katika Ligi. Wakati Chama, aliyewahi kuibeba Simba katika mechi nyingi kubwa za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa namba 10 katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mbali na hilo, Mwinyi aliishauri Yanga isibweteke na mafanikio yao kwa miaka ya hivi karibuni, bali iendelee kusajili wachezaji bora kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Mpira wa sasa hauwezi kumtegemea mchezaji mmoja. Hata kama Chama au Zouzoua wakifanya vizuri, bado timu inapaswa kuwa na mbadala wa uhakika. Michuano ya Afrika inahitaji ‘squad’ ndefu yenye wachezaji bora kila nafasi,” alisema Mwinyi.


Katika kipindi chake cha misimu mitatu Yanga, Aziz Ki alifunga jumla ya mabao 39 kwenye ligi na kutoa pasi 32 za mabao kwenye mashindano yote, na alitawala safu ya kiungo kwa umahiri mkubwa.

“Ni mchezaji wa kipekee, lakini mpira unakwenda mbele. Kama Yanga walimchukua kutoka ASEC na akafanya makubwa, basi na sasa wanaweza kumpata mwingine mzuri zaidi kutoka sehemu yoyote duniani,” alihitimisha Mwinyi.