Bruno apewa muda wa kufikiria

Muktasari:
- Inaelezwa matajiri hao wa Saudia wamewasilisha ofa ya Pauni 100 milioni kama ada ya uhamisho, pia wakiwa tayari kumpa mshahara wa Pauni 700,000 kwa wiki ikiwa pamoja na bonasi.
RIYADH, SAUDI ARABIA: MATAJIRI wa Saudi Araia, Al-Hilal wanadaiwa kuwasilisha ofa nyingine mpya na kumpa muda zaidi kiungo wa Manchester United, Bruno Fernandes kufikiria na kuamua ikiwa atakuwa tayari kujiunga nao katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa matajiri hao wa Saudia wamewasilisha ofa ya Pauni 100 milioni kama ada ya uhamisho, pia wakiwa tayari kumpa mshahara wa Pauni 700,000 kwa wiki ikiwa pamoja na bonasi.
Mabosi wa Al-Hilal wametoa wiki moja ya kujifikiria kwa Bruno kwa sababu inataka kumtumia kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu inayoanza mwezi huu.
Kocha wa Manchester United, ameweka wazi kwamba hafikiri ikiwa kiungo wake huyo atakuwa tayari kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi akiamini bado anahitaji kuendelea kusalia kwenye kikosi hicho.
Kwa mujibu wa The Mirror, Fernandes ambaye amepewa muda wa siku saba kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake. Wakala wake, Miguel Pinho, hivi karibuni alitumia siku tatu kwenye hoteli ya Four Seasons mjini Riyadh, ambako alifanya mazungumzo na wawakilishi wa Al-Hilal.
Katikati ya tetesi kuhusu hatima ya kiungo huyo, lejendi wa zamani wa Man United, Paul Scholes alisema timu yake hiyo inatakiwa umuuza Bruno kwa haraka kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kilichowekwa mezani kama ofa.
Scholes anaamini ikiwa Man United itaacha kuchukua kiasi hicho cha pesa, huenda isipate tena ofa kama hiyo kwa kuzingatia na umri ambao staa huyo anao.
Vilevile, Scholes amesema Man United inapaswa kumuuza mchezaji huyo kutokana na matatizo ya kifedha yanayoikabili timu hiyo baada ya kushindwa kutwaa taji dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye fainali ya Europa League na pia kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa hali iliyowapotezea mapato ya hadi pauni 100 milioni .