Aziz KI ampa mzuka Gomez

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Gomez alisema kitendo cha mchezaji huyo kutoka Ligi Kuu Bara kinaonyesha kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa zaidi, jambo linaloonyesha kuna mwanga mkubwa wa kufungua fursa kwa nyota wengine.
MSHAMBULIAJI wa Wydad Casablanca ya Morocco, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, amesema ni jambo zuri na la kifahari kucheza timu moja na aliyekuwa kiungo nyota wa Yanga raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz KI aliyejiunga hivi karibuni na kikosi hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gomez alisema kitendo cha mchezaji huyo kutoka Ligi Kuu Bara kinaonyesha kwa sasa Tanzania imepiga hatua kubwa zaidi, jambo linaloonyesha kuna mwanga mkubwa wa kufungua fursa kwa nyota wengine.
“Kiukweli kwangu ni fahari sana ingawa hatujapata muda wa kukaa na kuzungumza zaidi na kukumbushia maisha ya nyumbani Tanzania na soka letu la Afrika, napenda kucheza na wachezaji wakubwa kwa sababu ndio wanaoniongezea morali ya kupambana,” alisema.
Mshambuliaji huyo alisema licha ya umaarufu wa Aziz KI wakati akicheza Ligi Kuu Bara, lakini anapaswa kutambua katika kikosi cha Wydad kuna wachezaji wazoefu na maarufu zaidi, hivyo anatakiwa kupambana sana ili aendelee kuimbwa kama ilivyo kawaida.
“Kwa mfano kuna jamaa anaitwa Arthur Wenderroscky, raia wa Brazil, anajua sana na anacheza nafasi ambayo Aziz KI pia ana uwezo wa kucheza ipasavyo, huyo ni mmoja tu ila wako wengi, ni changamoto mpya kwake na anapaswa kuipambania,” alisema.
Akizungumzia michuano ya Kombe la Dunia la Klabu inayotarajiwa kupigwa huko Marekani kuanzia Juni 15 hadi Julai 13, mwaka huu, Gomez, alisema ni furaha kwake kwani itazidi kumuongezea motisha kutokana na wachezaji wakubwa atakaokutana nao.
Wydad iko kundi G la michuano hiyo na itafungua pazia Juni 18, kwa kucheza na Manchester City ya England, huku Juni 22 ikipambana na Juventus ya Italia, kisha kuhitimisha makundi kwa kupambana na Al Ain FC kutoka Falme za Kiarabu Juni 26.
Gomez alitangulia kujiunga na Wydad akitokea Fountain Gate, kabla ya Aziz kumfuata Mei mwaka huu akitokea Yanga.