Azam yatangulia fainali FA, goma la Yanga lavunjika

Daktari wa Yanga, Edward Bavu (kulia) akimpa huduma ya kwanza mwamuzi msaidizi, Charles Simon baada ya kupigwa jiwe na mashabiki wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jana. Mechi hiyo ilivunjika dakika 105. Picha na Doris Maliyaga
Muktasari:
Fujo kubwa zinazohisiwa kufanywa na mashabiki wa wenyeji Coastal kwa kurusha mawe, huku mchezaji Adeyum Saleh akipewa kadi nyekundu na mwamuzi msaidizi Charles Simon wa Dodoma kupigwa jiwe kichwani na mashabiki hadi kupasuka katika paji la uso, ni mambo yaliyochangia mchezo kuvunjika.
AZAM jana Jumapili bila kujali uchovu wa safari ya Tunisia ilipoenda kucheza na Esperance, ilitinga fainali ya Kombe la FA ikiing’oa Mwadui kwa penalti katika nusu fainali mjini Shinyanga, huku mechi ya Yanga na Coastal Union likivunjika jijini Tanga kutokana na vurugu za mashabiki.
Yanga na Coastal zilikuwa zikipepetana Uwanja wa Mkwakwani, lakini mechi ilivunjika dakika 15 kabla ya kumalizika 30 za nyongeza Yanga ikiwa mbele kwa 2-1.
Fujo kubwa zinazohisiwa kufanywa na mashabiki wa wenyeji Coastal kwa kurusha mawe, huku mchezaji Adeyum Saleh akipewa kadi nyekundu na mwamuzi msaidizi Charles Simon wa Dodoma kupigwa jiwe kichwani na mashabiki hadi kupasuka katika paji la uso, ni mambo yaliyochangia mchezo kuvunjika.
Coastal walioahidiwa Sh 40 Milioni wakiifunga Yanga walianza kupata bao dakika ya 53 kupitia Yousouf Sabo aliyefumua shuti kali lililomshinda kipa Deo Munishi ‘Dida’.
Donald Ngoma aliisawazishia Yanga dakika ya 60 akimalizia krosi, bao ambalo lililalamikiwa na wachezaji wa Coastal wakiamini mfungaji aliotea. Dakika 90 zikamalizika matokeo yakiwa 1-1 ndipo zikaongezwa 30 ambazo mashabiki wa Coastal walionekana kupinga na kutaka zipigwe penalti na dakika ya 101, Amissi Tambwe aliifungia Yanga bao la pili kabla ya kuzuka fujo uwanjani kiasi cha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatuliza mashabiki.
Hali ilikuwa tete zaidi baada ya Adeyum kumpiga kichwa mwamuzi msaidizi na kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi Abdallah Kambuzi na kusababisha vurugu kuongezeka huku mashabiki wa Coastal wakidai uwanja umejaa kiza.
Kamisaa wa mchezo, Osuri Kasuri, aliliambia Mwanaspoti kuwa mchezo ulivunjika kwa fujo za mashabiki wa Coastal na atapeleka ripoti TFF ili kuchukua uamuzi unaostahiki, ingawa matokeo yalikuwa mabao 2-1.
Yanga: Deo Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Kelvin Yondani/Malimi Busungu, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Ngoma/Tambwe, Haruna Niyonzima, Yosouf Boubacar/ Msuva.
Coastal: Fikirini Bakar, Hamad Juma, Adeyum Saleh, Hamid Mbwana, Miraj Adam, Abdulhalim Humud, Juma Mahadh, Yosouf Sabo, Ismail Mohammed, Gedfrey Wambura na Ayoub Yahya.
Azam ililazimika kusubiri mikwaju ya penalti kutinga fainali kwa kuing’oa Mwadui kwenye mechi ya nusu fainali nyingine ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
Hadi dakika 120 zinamalizika matokeo yalikuwa mabao 2-2, Azam wakiwa wa kwanza kuandika bao dakika ya tatu kupitia kwa Khamis Mcha ‘Vialli’ na Mwadui kusawazisha dakika ya 82 kupitia Salum Kabunda na kuupeleka mchezo muda wa nyongeza ambapo Vialli aliiongeza Azam bao la pili dakika ya 97. Wakati mashabiki wakiamini Azam imeshatinga fainali, Jabir Aziz aliisawazishia Mwadui kwa penalti na mchezo kuingia hatua ya kupigia penalti tano tano na Azam kuibuka na ushindi wa mabao 5-3.
Waliofunga penalti Azam ni Waziri Salum, Alan Wanga, Himid Mao, John Bocco na Aggrey Morris wakati waliofunga za Mwadui ni Jabir Azzi, Idd Mobi, Malika Ndeule wakati Kelvin Sabvato alikosa.
Baada ya kuvurugika mechi ya Yanga na Coastal, Azam sasa italazimika kusubiri kujua itacheza na nani fainali Mechi 28.