Azam yampotezea Diao, akitajwa APR Rwanda

Muktasari:
- Diao, alijiunga na Azam msimu uliopita Julai 4, 2023, kwa kishindo na kuonyesha kiwango bora chini ya aliyekuwa kocha Youssouph Dabo, alianza vizuri maisha ya Chamazi, huku akifananishwa kiumbo na mshambuliaji wa Kibelgiji, Romelu Lukaku.
MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Alassane Diao anaweza kutua APR FC ya Rwanda mara baada ya msimu huu kumalizika, kufuatia taarifa za kuaminika kueleza kuwa mabosi wa klabu hawapo tayari kumuongezea mkataba mpya straika huyo aliyekuwa na wakati mgumu tangu arejee kutoka majeruhi.
Diao, alijiunga na Azam msimu uliopita Julai 4, 2023, kwa kishindo na kuonyesha kiwango bora chini ya aliyekuwa kocha Youssouph Dabo, alianza vizuri maisha ya Chamazi, huku akifananishwa kiumbo na mshambuliaji wa Kibelgiji, Romelu Lukaku.
Uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi ulimfanya kuwa sehemu muhimu ya safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo.
Hata hivyo, baada ya kupata majeraha yaliyomweka nje kwa kipindi kirefu, nafasi yake katika kikosi cha kwanza ilianza kuyeyuka. Aliporejea, benchi la ufundi lilikuwa tayari chini ya Kocha Rachid Taoussi ambaye hakuonekana kumpa nafasi kama ilivyokuwa awali.
Kutokupata nafasi ya kutosha kumemvunja nguvu mshambuliaji huyo raia wa Senegal, ambaye sasa anatajwa kuwa na mpango wa kuondoka Azam mara baada ya msimu huu, huku APR FC ya Rwanda ikiwa ni moja ya klabu zinazotajwa kuhitaji huduma yake.
Kwa mujibu wa taarifa, APR tayari imeonyesha nia ya kumsajili Diao katika dirisha lijalo la usajili, wakitambua kuwa anaweza kujiunga nao kama mchezaji huru iwapo Azam itaendelea kumfungia vioo.
APR ambao ni mabingwa kihistoria Rwanda, inajipanga kwa msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa, hivyo wanatafuta wachezaji wenye uzoefu na ubora wa kimataifa kuimarisha kikosi chao, na jina la Diao limekuwa likitajwa kwa uzito.
Kwa sasa, Diao bado ni sehemu ya kikosi cha Azam, lakini amekuwa akipata muda mchache wa kucheza. Ukimya wa benchi la ufundi kuhusu mustakabali wake unazidi kuongeza uwezekano wa kuondoka kwake, hasa kwa kuzingatia kuwa klabu tayari haina mpango wa kumwongezea mkataba mpya.
Hadi sasa hakuna tamko rasmi kutoka kwa Azam wala Diao mwenyewe kuhusu suala hilo, lakini mazingira yaliyopo yanaelekea kuashiria kuwa safari ya mshambuliaji huyo ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaweza kufikia ukingoni mwisho wa msimu huu.