Azam inajaribu tena kutafuta rekodi Simba

Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo utakuwa ni kati ya wenyeji, Namungo wakiialika Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi.
Charles Abel, Mwananchi
Dar es Salaam. Ni mechi ya kisasi itakayochagizwa na vita ya kuwania ubingwa wakati Simba itakapoikaribisha Azam FC leo kwenye Uwanja wa Mkapa jijini kuanzia saa 1:00 usiku.
Wageni Azam wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na hamu ya kulipa kisasi cha unyonge wa misimu mitano mfululizo mbele ya Simba katika mechi za Ligi Kuu na imepoteza idadi kubwa ya mechi dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.
Katika misimu mitano iliyopita, timu hizo zimekutana mara 10 katika Ligi Kuu ambapo Simba imeibuka na ushindi mara tano, zikitoka sare mara nne huku Azam FC ikiibuka na ushindi mara moja tu.
Lakini ukiondoa hilo, mchezo wa leo ni muhimu kwa kila timu kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa kulingana na msimamo wa Ligi Kuu msimu huu ulivyo.
Wenyeji Simba walio na pointi 38, wanahitaji kushinda ili kupunguza pengo la pointi baina yake na Yanga kubakia pointi tatu huku pia wakibakiwa na mechi moja ya kiporo ambayo kama watashinda, watakwea kileleni mwa msimamo wa ligi lakini kama watapoteza maana yake watawafanya Yanga wawe na uhakika wa kubakia kileleni mwa msimamo wa ligi hata kama watakuja kushinda mechi yao moja ya kiporo itakayobakia baada ya mechi ya leo.
Kwa Azam walio katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi, ushindi leo utawafanya wafikishe pointi 35.
Ni mechi ambayo Simba itaingia ikiitegemea zaidi safu yake ya kiungo inayoundwa na wachezaji Lwanga Taddeo, Rally Bwalya, Luis Miquissone, Bernard Morrison na Clatous Chama ambayo ndio imekuwa muhimili wa kuifanya timu hiyo imiliki mpira, kutengeneza nafasi na kufunga.
Kwa upande wa Azam, yenyewe inawategemea zaidi washambuliaji wake, Obrey Chrwa, Mpiana Mozinzi, Prince Dube na Iddi Selemani ‘Nado’ kupeleka madhara langoni mwa Simba kutokana na makali yao ya kufunga.
Wakati Simba wakiingia wakiwa kamili katika mechi ya leo, Azam yenyewe itawakosa wachezaji watatu kutokana na sababu mbalimbali ambapo Yakubu Mohamed atakosekana kwa sababu ya kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano, Frank Domayo na Abdul Hamahama nado wagonjwa.
Kocha wa Simba, Didier Gomez alisema kuwa wanalazimika kushinda mechi hiyo ili wajiweke sawa kwa kisaikolojia kwa ratiba ngumu iliyo mbele yao ya ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.
Kocha msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati alisema kuwa timu yake iko tayari kwa mchezo huo na hawatishwi na ubora wa Simba.
Simba v Yanga yasogezwa mbele
Mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu baina ya Watani wa Jadi, Simba na Yanga, uliokuwa uchezwe Februari 20, umesogezwa mbele hadi Mei 8, saa 11 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) imeeleza kwamba mechi hiyo imeahirishwa kutokana na ushiriki wa Simba katika mashindano ya kimataifa ambapo ipo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi za mzunguko wa 19 zitaanza kuchezwa Februari 11, 2021 na Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika Juni 12, 2021.
Michezo ya mzunguko wa 19 ya Simba na Namungo FC imeahirishwa kutokana na ratiba za mashindano ya caf. Endapo Simba na Namungo zitafuzu kucheza hatua zinazofuata za michuano ya Caf, kuna michezo itaahirishwa kutoa nafasi kwa timu hizo kusafiri nje ya nchi.
Mchezo namba 208 wa mzunguko wa 24 kati ya Simba SC na Young Africans SC, utachezwa Mei 8, 2021, saa 11.00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa,” imesema taarifa hiyo.
Kuahirishwa kwa mechi hiyo kunaipa unafuu Simba, ambayo ilikuwa inakabiliwa na ratiba ya kucheza mechi tatu ngumu za Ligi Kuu na za Ligi ya Mabingwa Afrika ndani ya muda wa Siku 11.
Kwanza ni dhidi ya AS Vita huko DR Congo, Februari 12 na baada ya hapo ingeikabili Yanga, Februari 20 na siku tatu baadaye yaani Februari 23, ingekuwa na kibarua mbele ya Al Ahly ya Misri.