Aucho afunguka kabla ya kusajili Yanga
Kiungo mpya wa Yanga, Khalid Aucho wakati anatua Tanzania alikuwa aamevalia mavazi ya kujifunika huku akiwa pia amejiziba na barakoa licha ya kushangaa mabadiliko ya nchi akiushangaa pia Uwanja Mpya wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere 3 alisema amefurahi kurejea Tanzania.
Aucho alisema kuwasili kwake ni maalum kwa ajili ya kuja kumalizana na Yanga na kwamba atazungumza mipango yake hiyo baada ya dili hilo kukamilika.
“Nimefurahi kurejea hapa Tanzania hapa kwangu ni kama nyumbani si unajua hapa na nyumbani, naona mazingira yamebadilika sana sasa kuna Uwanja wa ndege huu mzuri na mkubwa, safi sana,”alisema Aucho.
“Siwezi kuzungumza sana kwa sasa meneja wangu alitangulia hapa ataweza kuongea zaidi lakini tutazungumza mara baada ya kumaliza kila kitu, acha kwanza nikapumzike.”
Ujio wa kiungo huyo sasa ni uhakika kwamba Yanga sasa itakuwa na mtu wa kushindana namba na Mkongomani Mukoko Tonombe lakini pia Aucho uhakika ataziba nafasi ya Mukoko katika mechi tatu za kwanza.
Mukoko alifungiwa kucheza mechi tatu kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika mchezo wa Fainali ya (ASFC) baada ya kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Simba John Bocco ambapo Yanga ililala kwa bao 1-0.
Kuwasili kwa Aucho sasa kunaifanya Yanga tayari imeshamalizana na mastaa watano wa kigeni huku wanne kati ya hao wakiwa tayari wameshafika nchini ambao ni washambuliaji Heritier Makambo,Fiston Mayele, kipa Diarra huku beki Djuma Shaban ambaye alishasaini akitarajiwa kuwasili nchini pekee.