Asante Kwasi apanguliwa kikosi cha Simba

Beki mpya wa Simba, Asante Kwasi
Muktasari:
wasi ambaye awali aliwekwa katika Hoteli ya Spice iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam juzi Jumanne aliwasili akitokea Iringa alikokwenda kukusanya kila kilicho chake na kujiunga rasmi na kambi hiyo
Beki mpya wa Simba, Asante Kwasi raia wa Ghana ameondolewa kwenye kikosi kitakachoivaa Ndanda FC ambayo ni mechi ya Ligi Kuu mzunguko wa 12 kwani hajafanya mazoezi ya pamoja na wenzake kutokana na kuchelewa kukamilika kwa usajili wake.
Usajili wa Kwasi ulikuwa na utata baada ya Simba kufanya mazungumzo na kumpa mkataba mchezaji huyo wakati bado ana mkataba na timu yake japokuwa baadaye walikaa mezani na kumalizana na klabu yake ya Lipuli FC.
Kwasi ambaye awali aliwekwa katika Hoteli ya Spice iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam juzi Jumanne aliwasili akitokea Iringa alikokwenda kukusanya kila kilicho chake na kujiunga rasmi na kambi hiyo ambapo leo Jumatano asubuhi alianza mazoezi ya ufukweni ambayo ni maalumu kwa ajili ya kumuweka fiti kabla hajajiunga na mazoezi ya pamoja na wenzake.
Simba chini ya Kocha Masoud Djuma, iliendelea na mazoezi yake katika uwanja wa Polisi, huku Kwasi akifanya mazoezi yake katika ufukwe wa Coco ambapo kocha Djuma aliliambia MCL Digital kuwa amemtengea mazoezi hayo maalumu na hatacheza mechi ijayo dhidi ya Ndanda FC.
Kwasi ataanza kuichezea Simba rasmi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo inatarajia kuanza hivi karibuni visiwani Unguja, Zanzibar.
"Ni mazoezi yake maalumu maana hajafanya mazoezi na wenzake hivyo ni lazima ajiweke fiti kwanza na mechi ijayo tutakayokwenda Mtwara yeye hatacheza, hayo mazoezi yatakuwa ya muda na atajiunga na wenzake," alisema Djuma
Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka leo Alhamisi kuelekea Mtwara ambako watacheza mechi hiyo ya ligi na baadaye kwenda Zanzibar kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi na ligi itasimama kwa muda.