Ambundo aibeba Dodoma Jiji kwa KMC

Muktasari:
- KMC sasa imepoteza mechi zote tatu ilizocheza kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Dodoma. Bao la Dickson Ambundo mwishoni wa kipindi cha kwanza, limeipa ushindi muhimu timu yake Dodoma Jiji kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC.
Ambundo alifunga bao hilo akipokea pasi nzuri ya Mcha Khamis baada ya kazi nzuri ya beki Abubakar Ngalema aliyepanda na mpira kwa kasi kabla ya kumfikia Mcha.
Bao hilo ni la nne kwa Ambundo ambaye anatarajiwa kujiunga na Yanga baada ya msimu huu kumalizika mwezi ujao, kufuatia mkataba wake wa msimu mmoja na Dodoma Jiji kuelekea ukingoni.
Ushindi huo umeifanya Dodoma Jiji kupanda hadi nafasi ya tano kwa alama 42 na kuishusha KMC iliyobaki na alama zake 41.
Kocha Habib Kondo wa KMC, amekiri timu yake kushindwa kabisa kufua dafu kwenye uwanja wa Jamhuri, akipoteza mchezo wa pili dhidi ya Dodoma Jiji pamoja na mwingine waliofungwa na JKT Tanzania.
"Mchezo ulikuwa mgumu sana wapinzani wetu wametumia nafasi waliyoipata huku tukishindwa kupata tena matokeo kwenye uwanja huu kwa mchezo wa tatu leo" alisema Kondo.
Upande wake Mbwana Makata, Kocha wa Dodoma Jiji alisema ushindi huo anaupeleka kwa wachezaji wake na mashabiki wa timu hiyo.