Aliyetishia Kariakoo Dabi mtandaoni adakwa na Polisi

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema shabiki huyo maarufu wa Simba alitoa kauli hizo na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Abdulshahib Hegga 'GB64' kwa tuhuma za kuhamasisha watu kufanya vurugu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba kesho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema shabiki huyo maarufu wa Simba alitoa kauli hizo na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa clip za video zilizosambaa mtandaoni zinamkariri shabiki huyo, akisema katika Dabi ya kesho Jumamosi na Simba kupoteza tena mbele ya Yanga, basi viongozi wa Simba hawatatoka salama uwanjani.

Muliro ametoa wito kwa mashabiki wa soka watakaoanzisha vurugu zozote au kujihusisha na vitendo vitakavyozua taharuki ndani au nje ya uwanja watashughulikiwa haraka kwa mujibu wa sheria.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalum linafuatilia kwa karibu sana mchezo wa soka unaotarajiwa kuchezwa kesho," amesema Kamanda Muliro na kuongeza;

"Kuelekea mchezo huo tumechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo, usalama siku ya mchezo utakuwa wa kiwango cha juu maeneo yanayozunguka uwanja nje na barabara za kuingia na kutoka uwanjani."

Muliro amesema ukaguzi utakuwa ni wa hali ya juu kabla ya kuingia uwanjani na haitaruhusiwa yeyote kwenda uwanjani na silaha ya aina yoyote isipokuwa kwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.

Yanga na Simba zitacheza kesho Jumamosi kuanzia saa 11:00 jioni mchezo wa duru la pili la Ligi Kuu Bara baada ya awali kukutana Novemba 5 mwaka jana na Vijana wa Miguel Gamondi kushinda mabao 5-1.

Ushindi huo ulisababisha aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' kufutwa kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Abdelhak Benchikha ambaye kesho itakuwa ni mara ya kwanza kuikabili Yanga katika mechi hiyo ya watani wa jadi itakayokuwa na 112 ya Ligi Kuu tangu ilipoasisiwa mwaka 1965.

Mchezo huo wa dabi umekuwa ukiteka hisia za mashabiki wengi nchini na nje ya nchi na hivyo usalama umekuwa ukiimarishwa.

Watetezi Yanga ndio kinara katika msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 55 baada ya michezo 21, huku Simba yenye alama 46 ikishika nafasi ya tatu kupitia michezo 20, nyuma ya Azam FC yenye pointi 51 kwa mechi 23 na timu zote zinawania ubingwa kwa msimu huu sambamba na kukata tiketi ya CAF.