Gamondi afichua jambo Yanga

Muktasari:

  • Baada ya kutolewa wiki chache zilizopita katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti, Yanga imeelekeza nguvu zake katika mashindano ya ndani ambapo ni kutetea mataji yake mawili, ligi na Kombe la Shirikisho (FA).

HESABU za Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mapema tu kadiri iwezekanavyo na ndiyo maana amefichua kuwa na dozi maalum kwa wachezaji wake kwenye uwanja wa mazoezi ili kila mmoja kuwa fiti na tayari kwa mchezo ambao atataka kumtumia.

Baada ya kutolewa wiki chache zilizopita katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti, Yanga imeelekeza nguvu zake katika mashindano ya ndani ambapo ni kutetea mataji yake mawili, ligi na Kombe la Shirikisho (FA).

Kocha huyo ambaye anafurahia upana wa kikosi chake na kile wachezaji wake wanachotoa, alisema mwezi uliopita (Aprili) ulikuwa mgumu kutokana na wingi wa michezo (6) ambayo ilikuwa mbele yao hivyo mabadiliko ya mara kwa mara kwa wachezaji kwenye kikosi chake cha kwanza ni jambo ambalo lilikuwa haliepukiki ili kutunza nishati ya kumaliza vizuri msimu.

"Tupo kwenye mwelekeo mzuri, bado tuna safari na tunatakiwa kupambana hatua kwa hatua na kupata matokeo mazuri katika kila mchezo ambao utakuwa mbele yetu ili kufanikisha malengo yetu, hatupaswi kuangalia nyuma tunajikita katika kile ambacho tunatakiwa kufanya," amesema kocha huyo.

Ndani ya michezo sita ambayo Yanga ilicheza Aprili, mmoja ulikuwa wa marudiano ya robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ambao ulimalizika kwa suluhu kisha mikwaju ya penalti iliwahukumu kwani ule wa kwanza jijini Dar es Salaam wiki moja nyuma mwishoni mwa Machi nao matokeo yalikuwa hivyo.

Baada ya kutupwa nje katika mashindano hayo ya kimataifa, Yanga ilirejea katika wimbi la ushindi kwa kuifunga Dodoma Jiji mabao 2-0 katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA), waliendelea kuzichanga pia karata zao vizuri katika michezo minne ya ligi kwa kuvuna pointi 10 kati ya 12.

Kibarua alichonacho Gamondi na vijana wake kwa sasa ndani ya Mei ni kusaka pointi 11 katika michezo sita yenye thamani ya pointi 18. Kwa kuvuna pointi hizo ina maana kuwa Yanga itatwaa ubingwa huo wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya 30 huku pia wakiwa na nafasi kwenye Kombe la FA.

Kwa sasa Yanga ambayo kituo chake kinachofuata ni Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 62 huku ikifuatiwa na Azam yenye pointi 54, Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 47.

Kwa upande wake kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amempongeza Gamondi kwa kazi nzuri na kubwa anayoendelea kuifanya kwenye kikosi hicho.

"Nadhani Yanga ina nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa, wanaonyesha kuendelea kukua."

Pluijm anatamani kuona Yanga ikifanya makubwa Afrika na uthubutu wa hilo anadai waliuonyesha tangu msimu uliopita kwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na msimu huu wamefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

SITA ZA YANGA

05.05.  Mashujaa v Yanga

08.05.  Yanga v Kagera Sugar

13.05.  Mtibwa Sugar v Yanga

22.05.  Dodoma Jiji v Yanga

25.05.  Yanga v Tabora United

28.05.  Yanga v Tanzania Prisons