Azam FC, Namungo mechi ya kisasi

Muktasari:

  • Mshindi wa mchezo huo ataenda kukutana na Coastal Union iliyoitoa Geita Gold kwa bao 1-0 katika hatua ya nusu fainali huku Ihefu iliyoitoa Mashujaa kwa penalti 4-3 baada ya suluhu dakika 90 itakutana na Yanga iliyoifunga Tabora United 3-0.

MCHEZO mmoja wa kukamilisha hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) utapigwa leo kati ya wenyeji, Azam FC itakayoikaribisha Namungo kuanzia sasa 1:00 usiku, mechi itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mshindi wa mchezo huo ataenda kukutana na Coastal Union iliyoitoa Geita Gold kwa bao 1-0 katika hatua ya nusu fainali huku Ihefu iliyoitoa Mashujaa kwa penalti 4-3 baada ya suluhu dakika 90 itakutana na Yanga iliyoifunga Tabora United 3-0.

Timu hizi zinakutana ukiwa ni mchezo tofauti kwa sababu ni wa mtoano ambapo Azam FC ilifika hatua hiyo baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 3-0, huku kwa upande wa Namungo ikiitoa Kagera Sugar kwa penalti 5-3 kufuatia suluhu dakika 90.

Azam inaingia katika mchezo huo ikimtegemea nyota, Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara tayari amehusika na mabao 20 akifunga 14 na kuchangia sita 'asisti' huku Namungo ikiongozwa na Pius Buswita mwenye matano.

Nyota wengine ambao wataongeza makali katika vikosi vya timu zote mbili ni Abdul Suleiman 'Sopu' na Ayoub Lyanga ambao wana mabao mawili kila mmoja wao kwenye michuano hii huku Namungo ikimtegemea mshambuliaji, Kelvin Sabato mwenye matatu.

Azam imekuwa tishio kwenye ufungaji wa mabao kwani ni timu inayoshika nafasi ya pili msimu huu ndani ya ligi kwa kufunga mabao mengi (50) nyuma ya Yanga inayoongoza na 55 huku ikiwa ya pili pia kwa kuruhusu mabao machache (16) nyuma ya Yanga yenye 12.

Kwa upande wa Namungo imekuwa haina uwiano mzuri kwenye kufunga mabao kwani hadi sasa imefunga 20 na safu ya eneo lake la ulinzi likiruhusu 23.

BATO IKO HAPA!

Katika mchezo huu bato itakuwa maeneo tofauti ambapo upande wa kulia wa Namungo inayomtegemea Hassan Kibailo itakutana na ushindani kutoka kwa winga, Kipre Junior huku Emmanuel Charles aliyewahi kuichezea Azam akikutana na Gibril Sillah.

Vita nyingine itakuwa kati ya beki wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes atakayekuwa kwenye wakati mgumu wa kupambana na Kelvin Sabato huku kiungo, Frank Domayo 'Chumvi' aliyepita ndani ya kikosi hicho akikutana na Feisal Salum 'Fei Toto'.

MBINU ZA MAKOCHA

Kocha wa Azam, Youssouph Dabo ni muumini sana wa kucheza soka la kushambulia huku akiitengeneza timu hiyo kupata mabao kupitia maeneo mbalimbali uwanjani tofauti na Kocha wa Namungo, Mwinyi Zahera anayetegemea mashambulizi ya pembeni mwa uwanja.

Zahera tangu atue ndani ya timu hiyo Desemba 30, mwaka jana akitokea Coastal Union amekuwa akitegemea mashambulizi ya pembeni kupata mabao akiwategemea Emmanuel Charles mwenye uwezo wa kukaba na mawinga, Hashim Manyanya na Hassan Kabunda.


MECHI YA KISASI

Mchezo huu utakuwa wa kisasi kwa Namungo kwani mara ya mwisho ilipocheza na Azam katika Ligi Kuu Bara ilifungwa mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi Aprili 14, mwaka huu yaliyofungwa yote na winga, Kipre Junior dakika ya 62 na 84.

Hata hivyo mechi ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Azam FC ilipoteza mabao 3-1 katika Ligi Kuu Bara Oktoba 27, mwaka jana yaliyofungwa na Pius Buswita, Hashim Manyanya na Reliants Lusajo huku la Azam likifungwa na Ayoub Lyanga.

Azam inapambana kupata taji hili kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo msimu wa 2018-2019 ilipoifunga Lipuli ya mkoani Iringa bao 1-0, huku kwa upande wa Namungo ikifika fainali ya michuano hii msimu wa 2019-2020 na kuchapwa na Simba mabao 2-0.

KAULI ZA MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo alisema anatarajia mchezo mgumu kwa sababu ni wa mtoano hivyo akitoa tahadhari kwa wachezaji wa timu hiyo kuongeza umakini kwani mara nyingi walizocheza na Namungo wamekuwa wakiwapa changamoto kubwa.

"Mchezo wowote wa mtoano huwa ni mgumu kwa sababu hata malengo ya timu yanabadilika kwenye aina ya uchezaji, nyota wetu tutakaowakosa kutokana na majeraha ni walewale wakiwemo, Sospeter Bajana, Allasane Diao, Franklin Navarro na Malickou Ndoye."

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera alisema wachezaji wote wako kwenye hali nzuri huku akiwataka kiwango walichokionyesha mechi yao ya mwisho na Simba dakika za mwishoni ndicho waendelee kukionyesha tangu mwanzo wa mchezo.