Aliyekuwa kocha Biashara atoa msimamo

Muktasari:
- Josiah aliiongoza Biashara msimu uliopita katika Ligi ya Championship akisaidiana na Edna Lema na Ivo Mapunda, kumaliza nafasi ya nne na kucheza hatua ya mtoano kuwania kupanda Ligi Kuu lakini ikafungwa na Tabora United mabao 2-1 na kuishia hapo.
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Biashara United ya Mara, Amani Josiah amesema kwa sasa yuko huru baada ya kumaliza mkataba na klabu hiyo huku akikiri kupokea ofa kutoka timu mbalimbali ambazo bado hajazitolea uamuzi akisubiri timu itakayomshawishi kwa ofa nzuri.
Josiah aliiongoza Biashara msimu uliopita katika Ligi ya Championship akisaidiana na Edna Lema na Ivo Mapunda, kumaliza nafasi ya nne na kucheza hatua ya mtoano kuwania kupanda Ligi Kuu lakini ikafungwa na Tabora United mabao 2-1 na kuishia hapo.
Kiwango kizuri kilichoonyeshwa na benchi hilo la ufundi kimezishawishi timu nyingi na tayari kocha msaidizi, Edna Lema ameshaondoka akibebwa na Yanga Princess ambayo imemrejesha kuinoa kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake.
Josiah aliliambia Mwanaspoti kwa sasa yuko kwenye mazungumzo na timu mbalimbali zikiwemo Songea United (zamani FGA Talents), Stand United ya Shinyanga na Biashara huku timu nyingine akiziweka kapuni lakini zote hajaridhishwa na ofa zao huku mazungumzo yakiendelea.
“Ni kweli nahitajika, kuna timu zimeniletea maombi zinahitaji nifanye kazi, nimepokea baadhi ya ofa zao, kuna wengine sijaingia nao kwenye mazungumzo wekiwemo hao Songea United, Stand United na hata Biashara lakini hakuna chochote tulichofikia hadi sasa,” alisema Josiah.
“Naendelea kukaribisha mazungumzo kwa sababu hakuna timu iliyo na uhakika hadi sasa. Mkataba wangu na Biashara United uliisha na wao nazungumza nao kama wengine, timu itakayokuja na pendekezo zuri na mazingira mazuri ya kufanya kazi nitakwenda huko.”
Mjumbe wa bodi ya Biashara Unted, Augustine Mgendi, alisema “Kwenye benchi la ufundi tuvute subira tutapeana ufafanuzi baadae kuna mambo tunaendelea nayo sidhani kama ni vizuri kulianzisha mapema. Tunataka tutengeneze idara zote twende nazo kwa umakini tuzikamilishe vizuri.”