Akpan aibukia beki

KWENYE mechi ya mwisho ya kirafiki juzi Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Alkholood, lakini kocha Zoran Maki alimfanyia mabadiliko mchezaji wake mpya, Victor Akpan.
Imezoeleka Akpan akicheza kiungo mkabaji na ilikuwa hivyo wakati wa kipindi cha kwanza, ila kipindi cha pili alicheza beki wa kati baada ya kutolewa Henock Inonga.
Akpan katika nafasi hiyo alicheza vizuri na kuimudu bila shida yoyote, huku akionekana kuwa na nidhamu kubwa ya ulinzi pamoja na maelewano mazuri na Joash Onyango waliocheza pamoja.
Kulingana na mabadiliko hayo ya nafasi kwa Akpan kutoka kucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi hadi beki wa kati halitakuwa jambo la kushangaza kwani inaweza kutokea siku moja benchi la ufundi likafanya hivyo kwenye baadhi ya mechi.
Alipoulizwa Akpan kutokana na mabadiliko hayo ya nafasi, alisema kikubwa anapambana na kuonyesha katika uwanja wa mazoezi ili kupewa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Alisema kocha ndiye anaona kwa kiasi kikubwa uwezo wa kila mchezaji na nafasi sahihi ya kumtumia, lakini kwa upande wake hana shida anaweza kucheza nafasi yoyote uwanjani.
“Wakati nikiwa mdogo nimewahi kucheza nafasi zote hadi kipa. Kwa maana hiyo ikitokea nimepangwa kama beki wa kati, kiungo au eneo lingine lolote nitafanya kazi yangu kama kawaida,” alisema Akpan.
“Ndio maana unaona baada ya kurudishwa katika nafasi hiyo ya beki wa kati nilicheza bila ya kuwa na shida yoyote kama nafasi yangu ambayo naitumikia kwa muda mrefu.
“Nakumbuka nikiwa Coastal Union kuna siku, ila sikumbuki tulicheza na nani, kocha Juma Mgunda aliwahi kunitumia katika nafasi ya beki wa kati dakika zote 90, nikamaliza mechi na akaniambia nimefanya vizuri,” alisema mchezaji huyo.
“Kikubwa kwangu naendelea kupambana kutafuta nafasi ya kucheza na benchi la ufundi lenyewe litafanya uamuzi wa nafasi ambayo nitafaa kucheza, kwangu wala haina shida.”