AKILI ZA KIJIWENI: Pengine Mghana wa Simba atakuja na jipya

Muktasari:

  • Simaanishi kwamba wachezaji kutoka Ghana huwa viwango vyao ni vidogo na haviwezi kusaidia klabu za hapa ila kinachonipa wasiwasi ni matendo na tabia zao za nje ya uwanja.

SIWASAGII kunguni wachezaji kutoka Ghana ambao wanakuja hapa nchini kucheza soka la kulipwa lakini kiukweli sajili zao huwa zinanipa shaka sana.

Simaanishi kwamba wachezaji kutoka Ghana huwa viwango vyao ni vidogo na haviwezi kusaidia klabu za hapa ila kinachonipa wasiwasi ni matendo na tabia zao za nje ya uwanja.

Wengi wao wanapokuja kucheza soka la kulipwa hapa huwa hawadumu kwa muda mrefu ama hawawi wachezaji muhimu katika kikosi na sababu kubwa huwa ni ufanisi mdogo ambao wamekuwa wakionyesha katika viwanja vya mazoezi.

Wakishakuja nchini na kuanza kulipwa fedha nyingi zaidi ya zile wanazopata kwao, husahau kile kilichowaleta na kuanza kupoteza muda na nguvu nyingi kwa mambo ya nje ya uwanja ambayo huwa hayana msaada kwao na badala yake yanawarudisha nyuma kama ulevi na uzinzi.

Kuna orodha ndefu tu ya wachezaji kutoka Ghana ambao licha ya kuja hapa wakiwa wametoka kufanya vizuri huko walikokuwa baada ya muda mfupi ya uwepo wao hapa, huanza kusotea benchi na wengine kutazama mechi wakiwa jukwaani.

Nimeziona tetesi za Simba kumhitaji mchezaji Derrick Fordjour anayecheza katika nafasi ya ushambuliaji kwenye kikosi cha timu ya Medeama inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana na mchezaji huyo ni raia wa nchi hiyo.

Niwe mkweli sijamfuatilia vya kutosha mchezaji huyo na kujiridhisha kuhusu kiwango na uwezo wake lakini Simba inafikia hadi inamsajili maana yake kuna vitu imeviona kwake na namba zake bila shaka zinashawishi.

Lakini ninapokumbuka historia ya maisha ya wachezaji wengi wa Ghana ambao huja hapa nchini, ninapata wasiwasi sana na usajili wa Fordjour kama kweli utafanywa na Simba labda aje kufanya kinyume na kile tunachomfikiria.

Kama atasajiliwa, Fordjour anapaswa kuhakikisha anafuta doa ambalo wachezaji wenzake kutoka Ghana wameliweka hapa nchini kwa kutumia muda mwingi zaidi kwa mambo ya nje ya uwanja na kushindwa kutoa mchango kwa timu zao.