Shabiki achomoa simu ya Mpanzu katika paredi
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea wakati wachezaji walipokuwa wakipanda mabasi yaliyokuwa yakiiongoza timu katika msafara wa kusherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
SHANGWE za paredi la ubingwa wa Simba zilivurugwa kwa dakika chache baada ya kiungo wa timu hiyo, Elie Mpanzu, kunusurika kuibiwa simu yake ya mkononi katika tukio lililotokea wakati wa maandalizi ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea wakati wachezaji walipokuwa wakipanda mabasi yaliyokuwa yakiiongoza timu katika msafara wa kusherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
Mpanzu ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji wa mwisho kupanda basi, alivamiwa na mmoja wa watu waliokuwa wamechanganyika kwenye umati wa mashabiki ambaye alifanya jaribio la kuondoka na simu yake ya mkononi.
Hata hivyo, kabla mtuhumiwa huyo hajatoweka, baadhi ya mashabiki pamoja na watu waliokuwa karibu walibaini tukio hilo na kumkamata.
Mtu huyo alizuiliwa papo hapo na kushambuliwa na wananchi wenye hasira kabla ya askari wa ulinzi kuingilia kati kudhibiti hilo.
Baada ya tukio hilo, simu ya Mpanzu ilirejeshwa salama kwake, kisha akaendelea na msafara wa paredi pamoja na wenzake.
Licha ya tukio hilo, shamrashamra za mashabiki wa Simba ziliendelea kama kawaida huku maelfu ya wapenzi wa klabu hiyo wakifurika barabarani kuisindikiza timu katika safari ya kusherehekea ubingwa walioutwaa baada ya kuifunga Azam bao 1-0 kwenye fainali iliyochezwa Zanzibar, jana Jumamosi.