Ajibu, Fei Toto shughuli pevu

Muktasari:
- Kitendo cha Yanga kupoteza pointi kwenye mechi, kunaweza kuisaidia Azam kupunguza pengo la pointi na hata kukaa juu ya msimamo wa Ligi Kuu.
YANGA imeendelea na mazoezi yake kujiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Biashara United utakaopigwa keshokutwa Alhamisi, lakini unaambiwa nyota wa klabu hiyo wakiwamo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Ibrahim Ajibu lazima wajipange baba’ake.
Unajua kwanini? Mara ya mechi hiyo ambayo itaamua hatma ya Kocha Mwinyi Zahera katika msako wa tiketi ya mechi za kimataifa mwakani, Yanga itakuwa na ratiba ngumu ndani ya Februari ikicheza mechi sita zitakazoamua mustakabali wake wa ubingwa wa Ligi Kuu.
Mechi hizo ndizo zimeshikilia hatma ya vinara hao wa Ligi Kuu kujua kama itabeba taji la 28 ama la!
Mazingira ya viwanja itakazoenda kucheza mechi hizo na tofauti ya pointi ilizonazo dhidi ya washindani wake ndio inayowafanya kina Fei Toto na Ajibu na wenzao kukaza msuli la sivyo itakula kwao mazima.
Changamoto ya kwanza inayoiweka Yanga kwenye wakati mgumu kuelekea mechi hizo ni ile ya viwanja kwani italazimika kucheza katika viwanja vinne tofauti ambavyo vimekuwa havina eneo zuri la kuchezea.
Viwanja hivyo vinaweza kuiumiza Yanga kwa namna moja au nyingine kwani italazimika kubadili mbinu zake za kiuchezaji tofauti na kutumia mbinu mbadala zitakazoifanya imudu aina hiyo ya viwanja vya mikoani.
Katika mechi hizo sita moja tu ni dhidi ya Simba ambayo Yanga itacheza Uwanja wa Taifa jijini huku nyingine za ugenini dhidi ya Coastal Union na JKT Tanzania (Mkwakwani Tanga), Singida United (Namfua-Singida) Mbao FC na Alliance zote za Mwanza.
Yanga itacheza mechi hizo ikiwa inakimbizwa kwa ukaribu na Azam yenye alama 47 zikipishana kwa pointi sita tu. Kitendo cha kuangusha pointi kwenye mechi hizo, kinaweza kuinufaisha Azam kutangulia Yanga na kujiweka kwenye nafasi ya kutwaa ubingwa.
Lakini pia inaweza kuwa faida kwa watani wao Simba ambao wanapaswa kucheza mechi sita za viporo ili kuwa na idadi sawa ya mechi za Yanga.
Kama Simba itacheza idadi sawa ya mechi na Yanga na ikiweza kuibuka na ushindi kwenye viporo vyake, itakuwa imezidiwa jumla ya pointi mbili ambazo zinaweza kuongeza presha upande wa Yanga.
Pamoja na hayo, kingine kinachoitega Yanga ni umbali na muda ambao itasafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine kucheza mechi zake.
Itaanzia Tanga kucheza na Coastal, Februari 3 na italazimika kutumia siku mbili kusafiri na kupumzika tayari kwa mchezo wake dhidi ya Singida United, Februari 6.
Ikitoka Singida itarudi tenaTanga kuikabili JKT Tanzania siku nne baadaye kisha itarudi jijini kucheza na Simba, Februari 16 na siku nne baadaye itakuwa jijini Mwanza kuikabili Mbao FC kabla ya kucheza na Alliance, Machi 2.
Kitendo cha Yanga kupoteza pointi kwenye mechi, kunaweza kuisaidia Azam kupunguza pengo la pointi na hata kukaa juu ya msimamo wa Ligi Kuu.
Azam awali ilizidiwa kwa pointi 11 na Yanga lakini kwa sasa imeweza kupunguza pengo la pointi hadi kufikia sita na hii ni kutoka na kichapo ambacho Yanga ilikipata kutoka kwa Stand United.
Kocha wa Azam FC, Hans Pluijm alisema ni mapema sana kwa sasa kutaja timu ipi itachukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.