Ajib, Barthez wapewa mchongo Ulaya

Ibrahimu Ajibu wa Simba.
Muktasari:
KWA sasa nchini kuna mzee mmoja anatembea kifua mbele kutokana na kuwa mzazi wa mchezaji pekee anayecheza soka la kulipwa Ulaya, Mbwana Samatta ambaye anakipiga KRC Genk ya Ubelgiji.
KWA sasa nchini kuna mzee mmoja anatembea kifua mbele kutokana na kuwa mzazi wa mchezaji pekee anayecheza soka la kulipwa Ulaya, Mbwana Samatta ambaye anakipiga KRC Genk ya Ubelgiji.
Baba mzazi wa Samatta, Mzee Ally Samatta amewatazama wachezaji watatu wa Simba, Yanga na Azam na kushangaa wanafanya nini nchini mpaka sasa wakati viwango vyao vinafaa kabisa kwenda kukipiga Ulaya kama mwanaye.
Samatta anakipiga Genk akitokea TP Mazembe ya DR Congo na tayari ameshafunga mabao mawili katika mechi sita alizocheza katika Ligi Kuu ya Ubelgiji ‘Jupiler League’.
Mzee Samatta ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, amewataja Ibrahim Ajib wa Simba, Ally Mustapha ‘Barthez’ wa Yanga na Farid Mussa wa Azam kuwa miongoni mwa nyota wanaomvutia sana na kwa viwango vyao na kudai kuwa anaamini wanaweza kuwa njia moja na Samatta kama wataendelea kukaza buti.
“Wapo wachezaji wengi kwa sasa wanaofanya vizuri na wana uwezo mkubwa wa kwenda kucheza nje, kikubwa ni kuzingatia tu misingi ya soka,” alisema Baba Samatta ambaye alikuwa akivalia jezi namba 10 kwenye kikosi cha Stars.
“Ninaweza kutaja watatu, kwa Simba kuna kijana anaitwa Ibrahim Ajib, ni mchezaji mzuri, anacheza soka la kuvutia na kutumia akili sana, anaweza kwenda kucheza nje kama atasimamia misingi ya soka.
“Kipa wa Yanga, Ally Mustapha (Barthez) na Farid Mussa wa Azam nao wana uwezo mkubwa wa kwenda kucheza nje, wana uwezo mkubwa,” alifafanua mzee huyo ambaye mwanaye mwingine ni Mohammed Samatta anayecheza Mgambo JKT.
“Farid ananikumbusha enzi zangu nikiwa nacheza soka, ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga chenga akiwa kwenye kasi, ni wachezaji wachache wenye uwezo huo,” aliongeza.
Ajibu, Barthez na Farid wamekuwa wachezaji muhimu kwenye vikosi vya timu zao msimu huu huku kila mmoja akifanya kazi kubwa kuhakikisha timu yake inafanya vizuri kwenye mbio za ubingwa.
Wakati huo huo wakala wa wachezaji nchini anayetambuliwa na Shirikisho la Vyama vya Soka Duniani (Fifa), Rahim Zamunda amewataja wachezaji Musa Nampaka ‘Chimbwabwa’ wa African Lyon na Miraji Athuman wa Toto African kuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye vigezo vya kwenda nje.
“Wapo wachezaji wenye uwezo huo, mfano Miraji Adam wa Toto, ana vigezo vyote na umri wake pia ni mzuri, anaweza kwenda Ulaya, yupo pia Chibwabwa wa hapa kwetu,” alisema Zamuga ambaye ni mmiliki wa African Lyon.