Aisha Masaka, Frida Amani waandaa mechi kuwabeba watoto wa kike

Muktasari:
- Mechi hiyo ya kampeni hiyo iliyoandaliwa na taasisi za wachezaji hao inatarajiwa kupigwa Juni 06, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge, jijini Dar es Salaam na utahusisha timu Aisha Masaka pamoja na ile ya timu ya Frida Amani ambapo mapato ya fedha yatakayopatikana yataenda kusaidia elimu mkoani wa Lindi.
NYOTA wa timu ya taifa ya Wanawake na klabu ya Brighton & Hove Albion ya England, Aisha Masaka akishirikiana na msanii wa hip hop, Frida Amani wamezindua kampeni ya 'Amka Malkia ' ya kumsaidia mtoto wa kike kutimiza ndoto itakayosindikizwa na mechi ya soka ya hisani.
Mechi hiyo ya kampeni hiyo iliyoandaliwa na taasisi za wachezaji hao inatarajiwa kupigwa Juni 06, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge, jijini Dar es Salaam na utahusisha timu Aisha Masaka pamoja na ile ya timu ya Frida Amani ambapo mapato ya fedha yatakayopatikana yataenda kusaidia elimu mkoani wa Lindi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo May 16, 2025, mastaa hao wanaosimama taasisi zao Aisha Masaka Foundation na Frida Amani Foundation, wamesema kampeni hiyo inatumia nguvu ya ushauri, ujumuishaji na fursa kuijenga ari ya kujiamini kwa wasichana na kufungua milango ya mafanikio.
Kwa upande wa Aisha, amesema ndoto yake ya kucheza mpira ilianzia akiwa shuleni, hivyo aliona ni vizuri kuanza kwa kusaidia Wanafunzi kupitia kampeni hiyo.
"Nitashirikiana na wachezaji wenzangu wa ndani na nje ya Tanzania kwa wachache watakaopata nafasi ambao hawatakuwa na ratiba za kubana katika klabu zao watashirikiana nami kucheza mechi hiyo ya Juni 6,2025," amesema Aisha.
Kwa upande wa Frida amesema, kuandaa mechi kubwa zaidi ni kumsaidia kumshika mkono mtoto wa kike kuweza kuishi na kutimiza ndoto zake.
"Amka Malkia ni wakati sasa wa mwanamke kujiamini na kujiongeza kwa kutimiza ndoto zao, kwa kile awalichokuwa akikitamani, siku hiyo mimi nitacheza soka, kitu ambacho watu wengi hawajui kama nina kipaji hicho, nitaandaa kikosi changu kitaingia nacho uwanjani ila najua timu Aisha Masaka tutawafunga magoli mengi tu," amesema Frida.