Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aisee Simba hii sasa sifa

Muktasari:

Simba ilianza kama utani msimu huu, lakini sasa imetimiza mechi 11 bila kupoteza mchezo na inavyoonekana hakuna timu ya kuweza kuizuia kwa sasa. Yanga ipo katika nafasi ya pili na pointi 21 na kwa hali ilivyo si rahisi kuifikia Simba hivi karibuni, japo ina mchezo mmoja zaidi mkononi.


KILA Ufalme una nyakati zake. Nyakati hizi ni za ufalme wa Simba na hilo limezidi kuthibitika baada ya juzi Jumapili kujipigia Toto Africans kwa mabao 3-0. Ushindi huo umeifanya ijiimarishe kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 29.

Simba ilianza kama utani msimu huu, lakini sasa imetimiza mechi 11 bila kupoteza mchezo na inavyoonekana hakuna timu ya kuweza kuizuia kwa sasa. Yanga ipo katika nafasi ya pili na pointi 21 na kwa hali ilivyo si rahisi kuifikia Simba hivi karibuni, japo ina mchezo mmoja zaidi mkononi.

Miongoni mwa vitu vinavyoibeba Simba msimu huu ni kuwa na kikosi kipana ambapo imekuwa na wachezaji ambao wakianzia benchi wanaweza kuingia kipindi cha pili kusaidia upatikanaji wa matokeo kama ilivyotokea katika mchezo wa Mbao FC ambapo Blagnon Frederick na Mohammed Ibrahim walifanikiwa kubadili mchezo.

Makala hii inaangazia mwenendo mzima wa Ligi Kuu na mambo ambayo yanazidi kujitokeza siku hadi siku.

 

Simba ililamba dume Mtibwa

Katika usajili wote wa Simba msimu, nyota watatu ambao iliwachukua kutoka Mtibwa Sugar wameonekana kuwa moto zaidi. Nyota hao ni Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin na Mohammed Ibrahim. Kichuya na Mzamiru tayari wameifungia timu hiyo mabao 11 huku wakihusika kutengeneza mabao mengine matatu. Kwa sasa hakuna ubishi kwamba nyota hao wamekuwa na kiwango bora zaidi Msimbazi. Ibrahim amekuwa akibadili upepo kila anapoingia jambo ambalo limeipa kiburi Simba.

 

Wazawa wanakaza

Ukiitazama chati ya wafungaji bora unapata picha halisi. Anayeongoza chati hiyo ni Shiza Kichuya ambaye kwao ni hapo Morogoro, halafu anafuatiwa na Rashid Mandawa mwenye mabao sita kisha Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting mwenye mabao matano sawa na Omary Mponda wa Ndanda halafu huko chini ndiyo utawakuta kina Chirwa. Katika vikosi vya kwanza vya timu nyingi wazawa wanaanza mbele ya wageni. Huu ni mwanzo mzuri kwa wachezaji wazawa ambao sasa wanampa kazi nyepesi kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa kupata wachezaji wa viwango vya juu.

 

Pluijm basi tu

Huenda itachukua miaka mingi kupata kocha mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza timu ya kushambulia na kufunga mabao mengi kama alivyoweza kufanya Hans Van Pluijm katika kikosi cha Yanga. Jumamosi iliyopita Yanga ya Pluijm iliongeza rekodi nyingine ya kupata ushindi mnono zaidi ugenini baada ya kuifunga Kagera Sugar kwa mabao 6-2 mjini Bukoba. Kabla ya hapo Pluijm aliweka rekodi ya ushindi mkubwa wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union na ule wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting. Habari mbaya ni kwamba mrithi wake, George Lwandamina tayari ametua nchini kuchukua mikoba yake.

 

Stand United bado moto

Yawezekana tulidhani ni nguvu ya soda lakini Stand United imedhihirisha kuwa imejipanga vizuri msimu huu baada ya kupoteza mchezo mmoja tu katika mechi zake 12. Kama sio makosa ya safu ya ulinzi, Stand ilikuwa imeshaiadhibu Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1, lakini baadaye mchezo huo ulikwisha kwa sare ya mabao 3-3 baada ya Mtibwa kusawazisha katika dakika za mwisho. Pengine moto uliowashwa na Stand utazidi kuchoma msimu huu na huenda ikamaliza katika nafasi nne za juu.

 

Mbeya City iko gonjwa

Wapenzi wa soka jijini Mbeya hawafahamu ni kitu gani kinatokea. Timu yao ya Mbeya City imekuwa nyanya na sasa inafungwa tu. Imefikisha mechi saba sasa bila kupata ushindi baada ya kufungwa mabao 2-0 na African Lyon Jumamosi iliyopita. Timu hiyo ya Mbeya ina kikosi kinachoundwa na wachezaji imara kama Rajab Zahir, Joseph Mahundi, Ayoub Semtawa na wengineo lakini wameshindwa kuwa timu ya ushindani. Kukosekana kwa straika mwenye uwezo mkubwa wa kupachika mabao kunaendelea kumgharimu kocha Kinnah Phiri.

 

Chirwa ameanza kujiamini

Wakati mwingine inahitaji roho ngumu kutetea uwezo wako. Obrey Chirwa baada ya kukaa miezi mitatu nchini bila kufunga bao lolote sasa amefunga mabao manne katika mechi tatu mfululizo. Ni uwezo wa juu. Chirwa alifunga mabao mawili dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi iliyopita na kuanza kuwaaminisha mashabiki wa soka nchini kuwa hakufanya makosa kuja kucheza soka la kulipwa nchini. Kwa sasa hata waliokuwa wakimbeza wameanza kupunguza maneno.

 

Mastraika Azam mmh!

Washambuliaji wa kati wa Azam, Gonazo Bi Ya Thomas, Fransico Zekumbawira na John Bocco wanazidi kumwangusha kocha wao Zeben Hernandez baada ya kucheza mechi tatu sasa bila kufunga bao la kawaida. Azam imepata mabao yake mawili ya mwisho kwa mikwaju ya penalti ambapo moja limefungwa na Himid Mao dhidi ya Mtibwa Sugar na nyingine na Bocco dhidi ya JKT Ruvu. Mastraika wa timu hiyo wanazidi kuwa butu kila uchwao jambo ambalo linamuweka katika wakati mgumu Hernandez ambaye anapigana kuokoa kibarua chake pale Chamazi.

 

Mabao kibwena

Wikiendi iliyopita ilikuwa na karamu ya mabao bhana, mechi nane zilizochezwa zilizalisha jumla ya mabao 27, huku hat trick ya kwanza ikipatikana msimu huu kwa mabao matatu ya Kelvin Sabato wa Stand United.

Mpaka sasa zaidi ya mabao 170 yamefungwa, huku Simba ikiongoza kwa mabao 21 ikifuatiwa na Yanga, huku Toto na JKT Ruvu zikiwa ndizo zenye mabao machache kuliko zote, kila moja ikiwa na mabao matano tu.