Afrika yote ipo Dar es Salaam

KUNA mechi tatu leo za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini Afrika yote macho na masikio yapo Dar es Salaam kwa Yanga na Mamelodi Sundowns katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 3:00 usiku, leo.

TP Mazembe na Petro Atletico zitamalizana mapema kabisa saa 10 jioni, baada ya hapo watu watavuta pumzi kidogo tayari kwa mechi kubwa halafu baadaye kabisa usiku mnene, Esperance itakiwasha na Asec Mimosas. Mechi ya Dar es Salaam imeteka hisia za wengi kutokana na kiwango bora ndani ya uwanja pamoja na mbwembwe za nje ya uwanja kwa timu hizo mbili ambazo rangi yao ya asili ni njano.

Yanga na Mamelodi Sundowns kila moja inaongoza msimamo wa ligi kuu nchini mwake huku na wachezaji wake mmoja mmoja wamekuwa na takwimu bora katika mashindano ya kimataifa, lakini hata kwa mikwara tu hawajambo.

Lakini sababu nyingine inayofanya mechi ya leo kuwa ya aina yake ni kumbukumbu ya miaka 23 iliyopita ambapo Yanga ilitolewa kwa kufungwa mabao 6-5 na Mamelodi Sundowns katika hatua za awali. Na sasa uwekezaji ambao Yanga wameufanya unawapa kiburi kwamba ni mziki tofauti kabisa ingawa kiuhalisia bado hawafikii hata nusu ya Mamelodi.

Yanga inaikabili Mamelodi ikitegemea zaidi makali ya safu yake ya kiungo ambayo imeonekana kuwa tishio katika hatua ya makundi ingawa wasiwasi upo katika safu ya ulinzi iliyoonyesha kusuasua kwenye hatua iliyopita.


PALE MBELE

Katika mechi sita za hatua ya makundi ya  mashindano hayo, Yanga imepachika mabao tisa ikiwa ni wastani wa bao 1.5 kwa mchezo na haikupata bao katika mechi mbili tu huku safu yake ya ulinzi ikiruhusu mabao sita sawa na wastani wa bao moja kwa kila mchezo.

Takwimu bora ambazo Mamelodi Sundowns wamekuwa nazo katika mashindano ya kimataifa  pindi wanapokuwa nyumbani, zinawalazimisha wachezaji wa Yanga kuhakikisha wanapambana kuibuka na ushindi leo iwe jua au mvua.

Kuna zaidi siku 1082 ambazo timu hiyo haijapoteza mechi yoyote ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ilikuwa mwenyeji na mastaa wao wamekuwa na morali na malengo ya juu sana wanapocheza mechi hizo.

Tangu ilipofungwa mabao 2-0 nyumbani na CR Belouizdad, Aprili 9, 2021, Mamelodi haijapoteza tena mchezo wa mashindano hayo ikiwa Afrika Kusini ambapo katika mechi 16 zilizofuata, imeibuka na ushindi mara 12, ikitoka sare nne, imepachika mabao 34 na yenyewe nyavu zake zimetikiswa mara tisa.


WAMISRI WABEBA LAWAMA

Mchezo huo utachezeshwa na marefa wote sita kutoka Misri ambapo wa kati atakuwa ni Amin Mohamed akisaidiwa na Mahmoud Ahmed na Ahmed Hossam huku kwenye chumba cha teknoklojia ya video ya usaidizi kwa marefa wakiwepo Mahmoud Ashor na Mahmoud Elbana.

Refa Amin anakumbukwa na wengi nchini kwani ndiye alichezesha mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 baina ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya DR Congo ambayo ilimalizika kwa sare tasa.


NOTI NJE NJE

Achana na fedha ambazo nyota wa Yanga watavuna kutoka klabuni kwao ikiwa itaibuka na ushindi leo, kuna uhakika wa zaidi ya Sh3 bilioni ikiwa itaitupa nje Mamelodi Sundowns na kutinga nusu fainali.

Ikiwa itatinga nusu fainali, Yanga itajihakikishia kiasi cha Dola 1.2 milioni (takriban Sh3 bilioni) ambazo ni fedha zitolewazo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kila timu ambayo itakomea katika hatua hiyo.


MOKWENA NA GAMONDI

Kila mmoja anamhofia mwenzie. Rhulani Mokwena anahofia uzoefu wa Miguel Gamondi ndani ya Mamelodi kwani aliwahi kuwepo miaka kadhaa iliyopita.

“Tunataka kufanya vizuri katika hatua ya mtoano, hiyo itatupa tathmini nzuri ya wapi tulipofikia. Tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo tupate matokeo mazuri ambayo ni muhimu. Ni mechi ngum u hasa kwetu lakini tutajitahidi kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Gamondi.

Kocha Mokwena wa Mamelodi Sundowns alisema,”Kwangu sijawahi kuutazama mchezo wa mpira wa miguu kwenye kujilinda zaidi (kupaki basi) bali nautazama mpira wa miguu kama burudani ambayo inapaswa kuambatana na matokeo mazuri.

Hakuna kitakachobadilika dhidi ya Yanga, kuhusu mbinu ni siri yangu na wachezaji wangu, naamini tuna kaka na dada wengi tu hapa Tanzania ambao watakuja kutushangilia.”


VITA YA WAZEE NA VIJANA

Ni dhidi ya wazee na vijana. Jana Simba imemalizana na Al Ahly, na leo Yanga itamalizana na Wasauzi kabla ya kwenda ugenini April 5-6 mwaka huu.

Hata hivyo baada ya matokeo ya jana kati ya Simba na Al Ahly. Presha imezidi kupanda kwa Yanga na Mamelodi kila timu ikiwaza itatoka vipi lakini kitu ambacho kinakoleza zaidi presha hiyo ni vita ya aina yake inayohusisha umri ambapo kila timu kuna eneo inakuwa mzee lakini wakati huo huo inakuwa kijana.

Eneo la kwanza ni la makocha wa timu hizo, Miguel Gamondi wa Yanga kwa sasa anaumri wa miaka 57 huku kocha mkuu wa Mamelodi Rulani Mokwena akiwa na umri wa miaka 37. Kwa hesabu za kawaida utaona wamepishana miaka 20 hivyo Gamondi ni mzee kwa Mokwena.

Hata kwenye tasnia ya ukocha, Gamondi ni Mzee ama baba kwa Mokwena kwani wakati Muargentina huyo anaanza kufundisha soka mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 33, Msauzi Mokwena alikuwa na miaka 11, akiwa hajui lolote kuhusu kuwa ukocha ila sasa ni mkali wa kazi hiyo kwa Afrika.

Aina hiyo ya ukinzani itanogesha zaidi mechi hii kwani kila mmoja atataka kuonyesha kuwa yeye kwa upande na umri wake ni masta katika kufundisha soka na kushinda mechi.

Eneo lingine ambalo litakuwa ni vita ya vijana na wazee ni uwanjani. Hapa Yanga imesheheni vijana kwenye kikosi chake hususani kile cha kwanza huku Mamelodi ikiwa na mafaza kibao kikosini.

Wastani wa kikosi cha kwanza cha Yanga cha sasa kina umri wa miaka 26 huku wastani wa umri wa kikosi cha Mamelodi ikiwa ni miaka 29.

Hivi ndivyo umri wa kikosi cha kwanza cha Yanga ulivyo; Djigui Diarra 29, Kouassi Attohoula 27, Joyce Lomalisa 30, Dickson Job 23, Ibrahim Hamad 26, Kharid Aucho 30, Mudathir Yahya 27, Stephane Aziz Ki 28, Maxi Nzengeli 24, Pacome Zouzoua 26 na Clement Mzize 20.

Kwa upande wa Mamelodi umri wa mastaa wa kikosi cha kwanza ni; Ronwen Williams 32, Khuliso Mudau 28, Grant Kekana 31,  Mosa Lebusa 31, Teboho Mokoena 27, Terrence Mashego 25, Thembinkosi Lorch 30, Peter Shalulile 30, Lucas Ribeiro 25, Themba Zwane 34, Gaston Sirino 33.

Kwa maana hiyo kikosi cha Yanga kitakuwa na faida ya kuwa na wachezaji wengi vijana ambao watakuwa na nguvu zaidi ya kupambana huku Mamelodi ikiwa na faida ya kuwa na mastaa wengi wazoefu.

Kocha mkuu wa Mamelodi, Mokwena alisema kuna siri kubwa kati yake na wachezaji kutokana na mbinu watakazozitumia leo na kuweka bayana kuwa hatapaki basi.

“Mbinu tutakazozitumia ni siri yetu kati yangu na wachezaji lakini tunatarajia kuwa na mechi nzuri ambayo itakuwa na ubora na yenye ushindani wa kutosha dhidi ya Yanga,” alisema Mokwena.

Gamondi wa Yanga alisema amekiandaa kikosi chake kushinda mchezo huo na kila mchezaji anatambua umuhimu wa mechi hiyo.

     “Ni mechi ngumu lakini tupo tayari kwa mapambano. Kila mmoja wetu anajua umuhimu wa kushinda mechi hii na sisi tumekiandaa kikosi kufanya hivyo,” alisema Gamondi.