Adel Zrane awaita mezani Simba

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kauli ya Zrane imekuja katika kipindi ambacho kumekuwepo na tetesi za Simba kuwa katika mpango wa kumrejesha Mtunisia huyo ambaye aliwahi kuitumikia timu hiyo wakati ilipokuwa ikinolewa na Patrick Aussems na baadaye Sven Vandebroeck na Didier Gomes da Rosa na kushinda nayo mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu.

MABOSI wa Simba wameng’atwa sikio na aliyekuwa kocha wao wa viungo, Adel Zrane akiwaambia wasifanye makosa kumuacha kocha Jadi Radhi ambalo wapo nalo mezani.

Radhi anatajwa kuwa yupo mbioni kumalizana na mabosi wa Simba kwa ajili ya kumrithi Robertinho.

Habari za ndani zinaeleza kuwa Mtunisia huyo huenda akatua kabla ya mechi yao ya Jumamosi itakayochezwa Uwanja wa Mkapa dhidi ya Asec Mimomas ikiwa ni mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na huenda wakamtangaza leo.

Mabosi wa Simba wanaelezwa kuwa wamekamilisha mchakato wote wa kocha huyo na kwasasa timu ipo chini ya Daniel Cadena aliyekuwa kocha wa makipa pamoja na Seleman Matola aliyekuwa kocha wa timu ya vijana.

Akizungumza na Mwanaspoti, Adel alisema anamfahamu Radhi kuwa ni kocha mzuri mwenye rekodi nzuri na mpira wa kuvutia na endapo Simba watakamilisha dili hilo basi atawafaa kwa sababu analijua soka la Afrika.

Adel ambaye pia anatajwa ndani ya Simba kurudi kuwanoa wachezaji wao alisema anamfahamu vizuri Radhi uzoefu wake kwani aliwahi kucheza pamoja na kufundisha.

“Ni kocha mzuri na aliwahi kuwa na Esperance ya Tunisia, alicheza Bolton kule Uingereza, anajua kuzungumza Lugha tatu (Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu); “Ikitokea tunafanya kazi pamoja ni kitu kikubwa kwangu na nina amini kabisa Simba itaenda juu zaidi, ujue hii timu inatakiwa iwe tano bora Afrika na kuendelea kukimbiza Afrika Mashariki.”

Adel akiwa na Simba amefanya kazi na makocha tofauti akianza na Patrick Aussems, Sven Vandebroeck na Didier Gomes huku mashabiki wakimsifia mitandaoni kwamba aliifanya timu hiyo kuwa kwenye fiziki nzuri tofauti na sasa.

Hata hivyo, Adel anaonekana zaidi kuwa chaguo na mashabiki wengi wa Simba kuhitaji arejee Msimbazi kwani kwenye kila posti yake katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakikomenti kumtaka aje Simba na wengine wamefikia hatua ya kuahidi kuchanishanga kumlipa wenyewe.

Adel alikiri kupokea ujumbe mbalimbali kutoka kwa mashabiki wakimuambia arudi kuokoa jahazi lakini yeye hana maamuzi ya mwisho mpaka viongozi wa klabu watakapomwendea hewani rasmi.

Adel alisema Tanzania ni nyumbani hivyo hawezi kujirejesha mwenyewe bila kufikia makubaliano lakini yupo tayari kufanya kazi tena nchini. “Napokea meseji nyingi sana kwenye simu yangu na hata mitandaoni, mashabiki wananiambia nirudi lakini siwezi kurudi tu mwenyewe, bado sijatafutwa na kiongozi kutoka kwenye bodi;

“Kocha wa makipa Dani (Cadena) na Matola (Selemani) nimekuwa nikizungumza nao mara kadhaa,”alisema na kuongeza kuwa suala la yeye kurejea nchini na kufanya kazi Simba sio ishu licha ya kwamba kwa sasa ana mkataba na APR Rwanda.

“Kweli nina mkataba hapa lakini ni mzuri kwangu na ninaweza kuondoka wakati wowote ule.”

Adel aliondoka Simba 2021 na sasa anatajwa kurejea kuja kuchukua mikoba ya Corneille Hategekimana ambaye alisitishiwa mkataba wake Novemba 7. Kocha huyo akiwa na Simba alikuwa sehemu ya ubora uliochangia kuchukua mataji ya Ligi Kuu mara tatu mfululizo na kufika hatua ya robo fainali ya Afrika.

Walati huo huo, mashabiki wa Simba jana walianza mkakati maalumu kwa kushirikiana na uongozi kuhakikisha timu yao inashinda dhidi ya Asec Mimosas kwa kishindo, jambo ambalo limewatia kiwewe Waivory Coast.