Yanga yapewa vigogo nane

Saturday June 25 2022
Nabi PIC
By Mwandishi Wetu

KIKOSI cha Yanga jana kilitua Mbeya na kupokewa kifalme na mashabiki waliofurika kwenye uwanja wa ndege kuwalaki mabingwa hao watakaocheza kesho mechi yao ya kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini ikiwa imeachiwa msala mpya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoshiriki msimu mpya.

Yanga imeshabeba ubingwa wa Bara mapema ikiwa na mechi tatu mkononi na juzi iliifunga Polisi mabao 2-0 na kesho Jumamosi itacheza dhidi ya Mbeya City katika mechi maalum ya kukabidhiwa ndoo yao kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kabla ya kurudi jijini Dar Juni 29 kumalizana na Mtibwa Sugar katika mechi ya kufungia msimu.

Kitendo cha kubeba ubingwa huo, ukiwa ni wa 28 kwao tangu ligi ya Bara ilipoasisiwa mwaka 1965 kimeifanya Yanga kupata tiketi ya michuano ya CAF, ikipangwa kucheza Ligi ya Mabingwa raundi ya awali, huku watani wao wakianzia raundi ya kwanza ya michuano hiyo itakayonza Septemba.

Uwepo wa idadi kubwa ya timu zinazoonekana kuwa imara kwenye raundi ya awali ya ligi hiyo, ni kama msala kwa Yanga na inailaizimisha timu hiyo kujipanga vilivyo ili iweze kuvuka raundi hiyo na kusonga mbele kuungana na Simba ambayo ni moja ya timu 15 zitakazokula shushu.

Yanga ipo katika nafasi ya 74 kwenye chati ya ubora ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutokana na uchache wa pointi ilizokusanya katika ushiriki wake wa michuano ya klabu Afrika katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni.

Nafasi hiyo imewanyima Yanga kuanzia hatua ya kwanza tofauti na Simba ambao wapo nafasi ya 15 na wataanzia raundi ya kwanza kama ilivyokuwa msimu uliopita ambao waling’olewa na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika na kukwamia robo fainali.

Advertisement

Tofauti na zamani ambapo hatua hiyo ya awali ilikuwa ikishirikisha timu nyingi zilizokuwa nyepesi kwa timu za Tanzania kupata matokeo mazuri na kufuzu hatua inayofuata, mambo yanaonekana sio rahisi kwa Yanga kutokana na uwingi wa timu nyingi ngumu katika hatua hiyo ambazo kama isipojipanga vyema zinaweza kuwavurugia mipango yao.

Baadhi ya timu ambazo kama Yanga inaweza kupangwa na moja kati ya hizo na pengine ikakutana na ugumu ni pamoja na Cape Town City ya Afrika Kusini, Primiero de Agosto na Petro Luanda (Angola), Asante Kotoko (Ghana), ASKO De Kara (Togo), CR Belouizdad (Algeria), CASA Sport (Senegal), Asec Mimosas (Ivory Coast) na Rivers United ya Nigeria.

River United ndio iliyoing’oa Yanga katika michuano ya msimu huu kwa kuifunga nje ndani kwa bao 1-0, hivyo kuitoa kwa jumla ya mabao 2-0.

Lakini ukiondoa hizo, zipo timu ambazo zinaonekana haziwezi kuwa mfupa mgumu kwa Yanga iwapo itakutana nazo kwenye hatua ya awali kutokana na kuwa na uzoefu mkubwa kuzizidi na hata mafanikio.

Ukiondoa sababu hizo, jambo jingine ambalo linaweza kuifanya Yanga kutokuwa na presha kubwa dhidi ya timu hizo ni ushindani mdogo na ubora wa ligi ambazo timu hizo zinatoka kulinganisha na Tanzania.

Klabu hizo ambazo hazionekani ni mlima mrefu kwa Yanga ni Horseed ya Somalia, SOAR Coyah (Guinea), Gaborone United (Botswana), Vipers (Uganda), Arta Solar (Djibouti), Eding Sport (Cameroon), APR (Rwanda), Watanga (Liberia) na Red Arrows ya Zambia.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema kuwa malengo yao ni kufanya vizuri pasipo kujali wanakutana na timu ipi, inga wa kwa sasa anaelekeza kwamba nguvu zake kukabidhiwa ndoo ya ubingwa wa Bara na kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi katika Ligi Kuu msimu huu.

Yanga haijaonja machungu ya vipigo tangu Aprili 25, 2021 ilipofungwa bao 1-0 na Azam katika ligi ya msimu uliopita na hadi sasa imetimiza mechi 35, ikisaliwa na michezo mitatu tu ifikie rekodi ya Azam iliyounganisha mechi za 38 za misimu mitatu, rekodi ambayo haivunjwa tangu mwaka 2015.


Advertisement