Yanga yajibu mapigo Simba

WAKATI mashabiki wa Simba na hata viongozi wake wakiamini, Yanga wana mechi nne nzito zinazoweza kuwashusha kileleni, wenyewe wamejibu mapigo, kwa kocha wao, Nasreddine Nabi kucheka sana na kisha akasisitiza hawabahatishi.
Iko hivi. Simba kupitia Mwenyekiti wao wa zamani, Ismail Aden Rage alisema kuna mechi nne ngumu ambazo anaamini zitaitoa Yanga kwenye mbio za ubingwa dhidi ya KMC, Azam, Simba na Mbeya City. Rage alisema; “Yanga wataanza kupotea dhidi ya KMC, Azam FC, Simba na Mbeya City wataambulia sare tayari mnyama atakuwa ametetea taji lake mara ya tano mfululizo hilo lipo wazi kutokana na timu hiyo kuwa wanyonge wa timu nilizozitaja pamoja na kupata matokeo mzunguko wa kwanza.” Alisisitiza kwa kujiamini kwamba kuteleza kwa Yanga kwenye mechi hizo kutairejesha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na kutetea ubingwa wao kwa mara ya tano mfululizo.
Leo Jumamosi Yanga itakiwasha na KMC kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, kisha ile na Azam itakayopigwa pia Dar Aprili 6, halafu Kariakoo Derby dhidi ya Simba Aprili 30 na mchezo mmoja kati ya mitatu ya ugenini dhidi ya Mbeya City.
Jeuri ya Rage na wanasimba imetokana na kuchungulia rekodi ya mechi baina ya timu hizo kwa miaka ya karibuni na kubaini ni ngumu Yanga kuzimaliza mechi hizo bila kutema pointi, japo katika mechi za raundi ya kwanza ilishinda kwa KMC na Azam, lakini ikatema pointi nne kwa Simba na Mbeya City kwa kutoka nao sare.
Kocha Nabi aliliambia Mwanaspoti kambini kwao Avic, Kigamboni juzi jioni kwamba, timu yake pamoja na uongozi wanatambua kwamba michezo hiyo ni migumu na mikakati tayari wanayo mkononi.
“Katika benchi letu na wasaidizi wangu, hata viongozi wangu hatujawahi kuwekeza nguvu kwa mechi hizo nne tu, sisi tunajua Yanga inacheza fainali 13 mpaka sasa,” alisema Nabi aliyeiongoza timu hiyo katika mechi 24 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu walipofungwa na Azam Aprili 25 mwaka jana, ambapo imecheza mechi 17 za msimu huu na saba za msimu uliopita ikigawa dozi au kulazimishwa sare tu.
“Kila mchezo kwetu ni fainali na kila mchezo una ugumu wake ukishadharau baadhi ya mechi utapata matatizo, akili yetu sasa utaona tunaiangalia KMC kwa umakini mkubwa na kujiandaa sawasawa kwa fainali hiyo. Tukimaliza mechi hiyo tutakuwa na mapumziko mafupi, lakini hapohapo tutaanza kujiandaa na fainali nyingine dhidi ya Azam na itaendelea hivyo hadi hesabu za ubingwa zitakapokuwa upande wetu.” “Yanga hatujawahi kuwa na mchezo rahisi kuna mambo mengi huwa yanatokea katika mechi zetu, hali hii inatufanya kuhakikisha tunakuwa katika umakini mkubwa katika kila mchezo na ndio maana tuko hapa tulipo. Tumekuwa tukifanya maandalizi makubwa mimi na msaidizi wangu Cedric Kaze kuhakikisha hatupotezi kasi ya malengo yetu katika msimu huu na kuendelea kutunza ubora wa kikosi chetu.”
Kocha alidai kwamba hakuna anayejua hesabu za Yanga ndio maana wapinzani wao wanazungumza mambo mengi ya kubeza uwepo wao kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.Katika mechi 13 ilizosalia nazo Yanga, tatu itacheza mkoani ambazo ni dhidi ya Biashara United, Mbeya City na Dodoma Jiji, wakati mechi nyingine 10 itacheza jijini Dar es Salaam ikiwamo dhidi ya KMC, Azam, Simba, Mbeya Kwanza, Ruvu Shooting, Polisi Tanzania, Namungo, Coastal Union, Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar,
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 45 ikifunga mabao 29 na kufungwa manne, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 37, huku Azam ikifuata nafasi ya tatu ikikusanya alama 28 kupitia mechi 18 ikiitangulia Namungo iliyoko nafasi ya nne.