Yanga ya ubingwa, Migne akeshea video

MASHABIKI wa Yanga bado wana presha kubwa, kiu yao ni kutaka kuona chama lao linarejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara walioupoteza tangu msimu wa 2017-2018 mikononi mwa Simba, lakini kumbe mabosi wao hawajalala kutokana na kulitengeneza benchi lao ili kurejesha heshima hiyo.

Mabosi hao wameamua kushusha makocha wapya wawili fasta, Mkenya Razack Ssiwa na Mfaransa Sebastien Migne ambaye anatarajiwa kutua nchini siku yoyote kuanzia leo Jumatatu na kulifanya benchi hilo sasa kuundwa na jeshi la watu nane wanaotoka mataifa matano tofauti, wakiwa na kazi ya kuipa Yanga ubingwa ndani ya miezi miwili iliyobaki kabla msimu wa 2020-2021 kumalizika.

Katika kuonyesha kuwa, Migne hana masihara, amekuwa akiiangalia video mbalimbali za mechi za Ligi Kuu Bara kupitia Azam Tv na akaunti yao ya YouTube ili kuwasoma kwa ukaribu zaidi vijana wake na wale wa timu pinzani.

Yanga ndio inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na alama 50 baada ya mechi 23, ikisaliwa na michezo 11 kumaliza msimu huku akili zao ni kutaka kuona wanatimiza lengo la kubeba ubingwa unaoshikiliwa na Simba waliopo nyuma yao na pointi 46 baada ya mechi 20 tu.

Mabosi wa Yanga wamekuwa wakifanya mambo yake kimyakimya na sasa uhakika kocha wao mpya Migne atatua wiki hii kuja kuanza kazi, lakini picha halisi ni kwamba benchi hilo litakuwa limesukwa na mataifa matano tofauti kutoka Afrika na Ulaya.

Ilianza na kumtanguliza kimyakimya kocha wa makipa Razack Ssiwa kutoka Kenya aliyeanza kazi tangu juzi akiwasha moto kwa makipa wawili huko Kigamboni uliowashtua mpaka mabosi wa timu hiyo, ambapo nyota wengi wa Jangwani wamekuwa wakinolewa na Juma Mwambusi.


BENCHI LILIVYO

Yanga sasa uhakika benchi lao litakuwa na wataalam watupu akianza Kocha Mkuu Migne ambaye Mwanaspoti linafahamu atakuwa nchini wakati wowote mapema wiki hii akitokea Ufaransa.

Migne ndio atakuwa raia pekee kutoka nje ya Afrika kuwa katika kikosi hicho huku wenzake wengine wote wakiwa raia wa Afrika ambapo chini yake atakuwa mzawa Mwambusi, aliyekomaliwa na mabosi hao abaki ili afanye kazi na Migne ikielezwa awali alitaka kuja na msaidizi wake.

Akitoka Mwambusi anafutiwa na Ssiwa raia wa Kenya ambaye sasa amepewa dhamana ya kuwanoa makipa wa timu hiyo, ambaye Mwanaspoti linafahamu amepewa kipengele kigumu katika mkataba wake akitakiwa kuhakikisha ndani ya miezi mitatu makipa wa timu hiyo wawe wamebadilika.


MGHANA NDANI

Chini ya Ssiwa kutakuwa na Mghana ambaye ni mtaalam wao wa viungo Edem Mortotsi ambaye juzi alirejea kazini baada ya mapumziko mafupi.

Mortotsi aliletwa na kocha aliyepita Cedric Kaze lakini mabosi wa Yanga waliamua kumbakisha sababu hakuonekana kuwa tatizo lililochangia kuporomoka kwa kiwango cha timu hiyo.


DAKTARI MZAWA

Yanga pia watakuwa na daktari mpya mzawa Nahumu Muganda waliyemchukua hivi karibuni kutoka Ihefu SC ya Mbeya akichukua nafasi ya Daktari mkongwe Shecky Mngazija aliyeomba kupumzika kwa muda majukumu ya klabu hiyo.

Benchi hilo pia litaendelea kupata huduma ya daktari wa viungo kutoka Afrika Kusini, Fareed Cassim ambaye amekuwa na umuhimu mkubwa katika kikosi hicho ambaye alikuja mapema katika utawala wa aliyekuwa kocha Mbelgiji wa timu hiyo Luc Eymael.


WENGINE NI HAWA

Benchi hilo linakamilishwa na Meneja Hafidh Saleh pamoja na Mtunza Vifaa, Mohammed Omar ambao wote ni wazawa na kukamilisha idadi ya wazawa wanne waliopo kwenye benchi hiyo wakiwa ni sawa na idadi ya wageni wakiongozwa na Migne.


TIZI LANOGA, SAIDO KAMA KAWA

Kikosi cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe ASFC dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa wiki ijayo, lakini mashabiki wamepata faraja baada ya kusikia na kumuona nyota wao, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akirejea uwanjani kwa kishindo kwa kufunga moja ya mabao yaliyoisaidia timu yake ya taifa ya Burundi, kupata sare nyumbani dhidi ya Jamhuri ya Kati na kuamini akirejea kikosini Jangwani mambo yatakuwa moto.

Saido aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu na kukosa michezo kadhaa ya Yanga, alifunga bao la kwanza na kuirejesha Burundi mchezoni mbele ya wageni wao waliokuwa mbele kwa mabao 2-0 na dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 2-2 na kumfanya mshambuliaji huyo kufikisha mabao manne akiongoza orodha ya wafungaji (kabla ya mechi za jana) sambamba na nyota wengine wa nchi za Afrika Kusini, Nigeria na Jamhuri ya Kati.

Wachezaji hao wenye mabao manne kama Saido kwenye michuano ya kufuzu AFCON ni Percy Tau (Afrika Kusini), Victor Osimhen na Alex Iwobi (wote wa Nigeria) na Luouis Mafouta ( Jamhuri ya Kati) aliyefunga mabao yote ya timu yake mbele ya Burundi.


WASIKIE WADAU

Wakati mashabiki wakijiandaa kupata raha kupitia benchi hilo jipya la Yanga, wadau mbalimbali wa soka akiwamo nyota wa zamani wa Simba, aliyewahi pia kukipiga Jangwani, Zamoyoni Mogella alisema Migne kufanya kile ambacho Wanayanga wanakitamani msimu huu itategemea na bahati tu.

“Amekuja katikati ya msimu, hivyo lazima atapitia kipindi kigumu, kufanya maajabu labda bahati imsimamie, sidhani kama programu zake zitaenda sawa kwa muda uliosalia, kwa kipindi hiki kwanza tumpe nafasi, tusije kuanza kumlaumu na yeye akaonekana hafai ndani ya muda mfupi,” alisema.

Alisema ujio wake ni sahihi, lakini Wanayanga wasimwekee matarajio makubwa msimu huu kwani kwake mafanikio yatatokana na bahati lakini wampe muda aandae timu ya ushindani msimu ujao.

Naye mchambuzi wa soka, Mwalimu Alex Kashasha, alisema ujio wa Migne sawa, lakini kwa Yanga bado mabadiliko ya benchi la ufundi sio suluhisho.

“Yanga iangalie katika haya makundi manne, menejimenti, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki, kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa asilimia 100? Kama kundi moja litatimiza na mengine yakashindwa maana yake ni tatizo,” alisema Mwalimu Kashasha aliyeffanua ndani ya msimu mmoja, Yanga imebadili makocha mara tatu, jambo ambalo kiufundi hata wachezaji linawavuruga.

“Migne anakuja akiwakuta wachezaji walewale, utamaduni wa Yanga ule ule hivyo atahitaji muda zaidi na wakati huo Ligi inaendelea, atataka kuisoma timu, malengo yao, aina ya wachezaji aliowakuta, nguvu ya wapinzani wao wote katika Ligi, utamaduni wa klabu na yeye pia atakuja na falsafa yake,” alisema Kashasha.