Watano wapya Simba iwe fursa kwa Sven

Thursday November 19 2020
sven pic

Pazia la mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika limebakiza siku chache kufunguliwa kwa timu wawakilishi wa nchi ikiwamo Tanzania Bara kuanza harakati za kuwania ubingwa.

Simba, mabingwa wa Ligi Kuu Bara itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Namungo wakitua Kombe la Shirikisho kufuatia kuibuka washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba walioibuka mabingwa wa kombe hilo. Wakati timu hizo zikiwa katika harakati za kujisuka, tayari Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limeshazijulisha kwamba timu ipi itakutana na ipi katika hatua hizo za awali za mashindano hayo.

Mbali na kutoa ratiba, Caf wakaenda mbali zaidi na kuziangalia timu zote shiriki kusoma alama za nyakati na kugundua kwamba bado dunia inapambana na maradhi ya Covid 19 ambayo sio tu Ulaya, bali hata Afrika kuna nchi mbalimbali hali bado haijatulia.

Kuliona hilo tayari Caf imeshatoa mustakabali kwa klabu zote ikitoa fursa ya kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya wachezaji kwa vikosi vyote shiriki kutoka 30 mpaka 40 kutokana na kuwepo kwa vipimo vya Covid 19 ambavyo wakati mwingine timu inaweza kujikuta inapoteza wachezaji wengi endapo watagundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Simba na Namungo zimepokea ujumbe huo na tayari klabu ya Simba kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘MO’ ameshalitolea ufafanuzi hilo kwamba wanachosubiri ni mwongozo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwawashia taa ya kijani juu ya usajili huo unavyotakiwa kufanyika na utakuwa na masharti gani.

Binafsi hii inaweza kuwa njia ya kwanza kwa Simba kujipanga vyema kwa kuboresha zaidi katika kufikia malengo yao na hata nchi kwa ujumla kwa kuhakikisha wanaingiza majina muhimu yenye ubora kwenye mashindano hayo makubwa.

Advertisement

Soka ni mchezo wa wazi hata kama Simba inaonekana kuwa na kikosi bora, lakini mashaka yapo wazi kwamba kikosi hicho kinahitaji maboresho makubwa ili kuwa wawakilishi bora kwenye anga ya kimataifa.

Simba inatakiwa kukumbuka kwamba kwanza fursa hii haiwagusi wao peke yao, bali hata klabu kubwa na wapinzani wao nao wanakutana nayo, na bahati mbaya huko kwa wenzetu hawana siasa kama zetu wanafikiria zaidi mafanikio kama taifa kuliko mafanikio binafsi.

Akili ninayoitegemea hapa ni kuona Simba inatulia na kwanza kwa umuhimu wa kipekee wanatanguliza heshima kwa kocha Sven Vandenbroeck ambaye kimsingi ndiye ambaye anajua wapi kunahitajika ongezeko la mchezaji gani na achukuliwe wa aina gani.

Heshima hiyo haitakiwi kuishia hapo tu, bali pia inatakiwa kwenda mbali zaidi kwa kumshirikisha hata katika wachezaji ambao viongozi watawapata ili apime kweli mchezaji husika anakidhi kiwango cha kuongeza kitu katika timu yake au vinginevyo.

Nasema hivi kwa sababu kupitia fursa hii wapo wajuaji wengi wa soka watajitanua na kutafuta wachezaji wao badala ya kuzingatia zaidi mahitaji ya timu na ushauri wa kiufundi kutokana na makocha ndio mwisho wa siku watakuja kubeba lawama za wajuaji hao.

Simba inatakiwa kutuliza akili eneo hili kwani makosa yatakayofanyika hapa yataondoa maana nzima ya fursa hii na badala yake litageuka janga kwa kuikandamiza timu husika katika kupata matokeo yaliyo mabovu.

Kinachoonekana haraka ndani ya kikosi cha Simba mbali na upungufu wa kiufundi lipo pia tishio la majeruhi na linaweza kuwa janga lingine ambalo litawalazimu viongozi wa Simba kujaribu kutanguliza utulivu kuliko ubishani wa ujuaji katika usajili huu muhimu.

Nimeona niimulike zaidi Simba kutokana na hulka ya klabu hizi kubwa katika eneo hili la usajili inawezekana ndio wakati ambao huibuka mambo ya hovyo yanayokosa weledi na wakati mwingine kuzibomoa timu katika kupata vikosi bora.

Ni vyema sasa ukomavu wa Simba ukaanza kuonekana hapa ili waweze kufikia malengo yao.

Advertisement
​