VIDEO: Ndayiragije hawatoa hofu Watanzania Taifa Stars itapindua meza kwa Sudan

Muktasari:

Tanzania watakuwa wageni wa Sudan kwenye Uwanja wa El Merreikh Omdurman, Khartoum huku wakihitaji ushindi wa 2-0 ili kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika Tanzania kufungwa 1-0.

Omdurman, Sudan. Kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa Tanzania 'Taifa Stars', Etienne Ndayiragije amewatoa presha mashabiki wa Tanzania kwa kusema wana kila sababu ya kupindua matokeo kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

Tanzania watakuwa wageni wa Sudan kwenye Uwanja wa El Merreikh Omdurman, Khartoum huku wakihitaji ushindi wa 2-0 ili kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika Tanzania kufungwa 1-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ndayiragije alisema mchezo uliopita wameona sehemu gani ya kuanzia katika mchezo huu wa marudiano.

"Katika mchezo uliopita tulimiliki mpira, lakini tulishindwa kufunga na changamoto hiyo tayari tumeshaifanyia kazi hivyo naamini kabisa tutatoka na ushindi, vijana wana morali na nimewaambia wanatakiwa wawe watulivu" alisema.

Akizungumzia changamoto ambazo amekutana nazo nchini Sudan alisema jambo kubwa ni viwanja wa kufanyia mazoezi kutokuwa na ubora wa kutosha.

"Unajua sheria unatakaiwa utumie uwanja wa mechi siku moja kabla ya mchezo kwahiyo tulikuwa tunatafuta viwanja vingine, lakini vinakuwa vibaya kwenye pichi najikuta nahofia kuwaumiza wachezaji wangu, sehemu zao za kuchezea zimekauka sana," alisema Mrundi huyo.

Tshabalala hatihati

Kocha Ndayiragije alisema katika kikosi chake ana majeruhi mmoja beki Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Etienne alisema aliamua kumpumzisha mchezaji huyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda baada ya kupata maumivu kabla ya mchezo huo.

"Tshabalala aliumia kabla ya mchezo wetu wa kirafiki ndio maana niliamua nimpumzishe, lakini tulipofika hapa alifanya mazoezi kidogo na yeye mwenyewe anasema yupo fiti kwahiyo nitamuangalia katika mazoezi ya leo jioni," alisema.

Nyoni ala kiapo

Nahodha msaidizi wa Stars, Erasto Nyoni amesema wachezaji wote wamesema wanahiaji kupata matokeo mazuri katika mchezo huu.

"Tunaomba watanzania wa dini zote watuombee kwasababu sisi ndio tupo huku tunawawakilisha, naamini kabisa tutafanya vizuri kwa niaba yao," alisema Nyoni.

TFF watia neno

Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani alisema kwa upande wao wamefanya kila linalowezekana kuhakikisha timu hiyo inafana vizuri.

Nyamlani alisema walihakikisha timu hiyo inafika sehemu nzuri, mechi za kirafiki na vitu ambavyo vitawafanya wachezaji kujiskika huru.

"Sisi tupo pamoja na vijana wetu wazalendo, tumehakikisha wanapata kila ambacho wanahitaji (stahiki zao) kwahiyo nina imani hakuna kinachokwamisha ushindi," alisema Nyamlani.