VIDEO: Kocha Tanzania aingia na mfumo wa 4-5-1 kwa Sudan kesho

Muktasari:

Tanzania inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao mawili katika mchezo huo ili kupata nafasi ya kufuzu kwa Chan2020 Cameroon.

Omdurman, Sudan. Kaimu kocha mkuu wa Tanzania, Etienne Ndayiragije alikuwa akitumia mfumo wa 4-5-1 katika mazoezi yake ya mwisho usiku huu akijianda na mchezo wa kesho Ijumaa dhidi ya Sudan.

Katika mazoezi yanayoendelea usiku huu kwenye Uwanja wa El Merreikh Omdurman, Sudan kocha huyo alipanga vikosi viwili alikuwa akitumia mfumo wa 4-5-1, lakini hapo hapo akichanganya 4-4-2 wakati kwa upande wa kikosi ambacho kilikuwa hakijavaa bips kilikuwa kikicheza 3-5-2.

Katika mfumo wa 4-5-1 kocha huyo aliwatumia Erasto Nyoni, Bakari Mwamnyeto, Gadiel Michael, Salum Kimenya, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Frank Domayo, Idd Nado, Miraj Athuman na Ditram Nchimbi.

Nchimbi akiwa mshambuliaji pekee wa kati aliyeanza huku akisaidiwa na Miraj na Nado wanaotokea pembeni katika kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi wanazopata.

Ushambuliaji alikuwepo Ditram Nchimbi, yeye alikuwa anatakiwa kutumia nguvu nyingi kuingia katika safu ya ulinzi iliyokuwa inaongozwa na vijana Oscar Masai na Dickson.

Katika mfumo wa 4-4-2 na 3-5-2 kocha huyo aliwaanzisha mbele Shabaan Chilunda pamoja na Kelvin John na kazi ngumu kuhakikisha anapenya katika safu ya ulinzi iliyokuwa inaongozwa na Erasto Nyoni pamoja na Bakari Mwamnyeto.

Chilunda na Kelvin walikuwa wanacheza kwa maelewano kwani kama mmoja alikuwa anaenda kukaba basi atamwambia mwingine abaki.

Katika kikosi cha pili kilikuwa na Oscar Masai, Dickson Job, Boniface Maganga, Abdulaziz Makame, Mudathir Yahya, Salum Abubakari, Hassan Dilunga, Shaban Chilunda na Kelvin John.

Mazoezi haya walikuwa wanacheza kwa kuangalia namna ya kupenya nguzo za timu pinzani huku timu zote zikitumia pembeni kupenya.

Katika eneo la viungo walikuwa wanacheza kwa kugusa mara mbili na pasi ya tatu walikuwa wanahakikisha wameshasambaza mipira.

Sehemu hiyo ilikuwa ikisimamiwa vizuri na benchi nzima la ufundi ambalo lilikuwa limesimama kwa mafungu mafungu.