Stars kupindua meza kibabe

Muktasari:

Stars katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri leo walianza kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa ya Rwanda ugenini, mchezo uliomalizika kwa suluhu.

KIKOSI cha timu ya taifa 'Taifa Stars', leo Ijumaa kitashuka dimbani kucheza na Sudan ukiwa ni mchezo wa kuwania kufuzu fainali za CHAN ambazo zinatarajiwa kufanyika nchini Cameroon.


Michuano hiyo inashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani ambapo Stars wapo ugenini jijini Khartoum, Sudan na mechi hiyo itachezwa saa 1:00 usiku.


Katika mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Stars walikubali kipigo cha bao 1-0, kwa maana hiyo mechi ya leo wanahitaji ushindi wa kuanzia mabao mawili au kama watashinda bao 1-0, watakwenda katika hatua ya mikwaju ya penati.


Stars inapaswa kupambana zaidi kwani wakipata matokeo tofauti na hayo basi safari yao itakuwa imeishia hapo.


Stars katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri leo walianza kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa ya Rwanda ugenini, mchezo uliomalizika kwa suluhu.


Wakati Stars wakiingia kusaka matokeo ya kusonga mbele kwenye mchezo huo benchi la ufundi la timu hiyo litakuwa na kibarua kingine kigumu kwani mechi zao sita ambazo wamecheza hakuna hata mechi moja waliyopata ushindi ndani ya dakika 90, lakini wakiwa wamefunga mabao mawili tu.


Stars chini ya mkuu wa benchi la ufundi Etienne Ndayiragije pamoja na wasaidizi wake Seleman Matola na Juma Mgunda wamecheza mechi sita wameshindwa kupata ushindi ndani ya dakika 90, dhidi ya Kenya na Burundi, walifungwa na Sudan, suluhu na Rwanda.