Vipigo bila huruma Ligi Kuu England

Muktasari:
- Kila msimu kwenye Ligi Kuu England imekuwa ni kawaida kushuhudia mechi moja timu ikipigwa bao nyingi, yakiwamo yale matokeo ya 8-2 ambapo Manchester United iliwahi kujipigia Arsenal.
LONDON ENGLAND. LIGI Kuu England inarudi wikiendi hii na bado hakujashuhudiwa kipigo cha mabao mengi yenye kuvunja rekodi kwenye mechi moja.
Kila msimu kwenye Ligi Kuu England imekuwa ni kawaida kushuhudia mechi moja timu ikipigwa bao nyingi, yakiwamo yale matokeo ya 8-2 ambapo Manchester United iliwahi kujipigia Arsenal.
Hata hivyo, kwenye Ligi Kuu England kuna mechi tano zilizoweka rekodi ya kushuhudia timu ikipigwa mabao mengi katika historia ya ligi hiyo iliyoanza 1992. Mechi zinazoshika rekodi ya kipigo kizito ni hizi hapa, je zitavunjwa rekodi hizi?
5.Chelsea 8-0
Aston Villa
Desemba 23, 2012, Chelsea walitaka kuvunja rekodi yao ya mabao kuichapa timu moja kwenye Ligi Kuu England, lakini wakashindwa na kuifikia tu.
Chelsea walikuwa kwenye ubora mkubwa kweli kweli wa kutikisa nyavu kwenye mechi hiyo wakati walipotupia kwenye nyavu za Aston Villa mara nane, wakishinda 8-0.
Mabao ya The Blues kwenye mechi hiyo yalifungwa na Ramires, aliyepiga mbili, huku Hazard, Oscar, Lampard, Torres, David Luiz na Ivanovic kila mmoja alipiga moja. Mechi ilikuwa kiwango bora cha timu nzima.
4.Chelsea 8-0 Wigan
Mei 9, 2010, Chelsea walitaka kumaliza msimu wakiwa kwenye kiwango cha juu wakati waliposhusha kipigo kizito kwa Wigan Athletics.
Katika mechi hiyo iliyofanyika uwanjani Stamford Bridge, Chelsea walipiga mtu 8-0 na kufuta matumaini ya Manchester United kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu England.
Mechi hiyo ilishuhudia mabao ya Didier Drogba, akifunga hat-trick na akabeba Kiatu cha Dhahabu kwenye mechi hiyo, Anelka alipiga mbili, Frank Lampard alifunga kwa penalti na Kalou na Ashley Cole nao waliweka mipira nyavuni kwenye mechi hiyo.
3.Tottenham 9-1 Wigan
Novemba 22, 2009, Tottenham Hotspur waliisasambua Wigan Athletics 9-1 uwanjani White Hart Lane.
Kikosi hicho chenye maskani yake London walicheza mchezo mkubwa kweli kweli si tu kufunga tu mabao peke yake.
Katika mechi hiyo ilishuhudia mchezaji mmoja akipiga Bao Tano peke yake na huyo mtu alikuwa Jermaine Defoe.
Wafungaji wengine katika mechi hiyo ni Crouch, Lennon, Bentley na Kranjcar, ambao kila mmoja alifunga bao moja. Scharner alifunga bao la kujifariji la Wigan.
2.Newcastle 8-0 Sheffield Wed
Septemba 19, 1999, Newcastle United iliifanyia maangamizi ya kutisha Sheffield Wednesday kwa kuwachapa 8-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu England.
Katika mechi hiyo, straika Alan Shearer alifunga mabao matano, ikiwamo mawili ya penalti. Hughes, Dyer na marehemu Gary Speed walifunga bao moja moja kila mmoja.
Hiyo ndiyo mechi inayoshika namba mbili kwenye Ligi Kuu England kwa kushuhudia timu moja ikiichapa timu nyingine mabao mengi.
1.Man United 9-0
Ipswich Town
Machi 4, 1995, Manchester United iliweka rekodi ya kuwa timu iliyoshinda mabao mengi zaidi kwenye mechi moja ya Ligi Kuu England.
Rekodi hiyo ilikuja kwenye mechi ambayo waliichapa Ipswich Town 9-0. Staa matata katika mchezo huo alikuwa Andy Cole, ambaye alifunga mabao matano, Mark Hughes alipiga mbili huku Paul Ince na Roy Keane walifunga bao mojamoja kila mmoja.
Lakini, cha ajabu msimu huo ubingwa ulibebwa na Blackburn Rovers.