Tiketi ya Simba CAF ipo Dar

SIMBA juzi ilipoteza mechi yake ya pili katika Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa na Asec Mimosas na sasa imesalia na dakika 90 za maajabu Dar.
Wawakilishi hao wa Tanzania ilifungwa mabao 3-0 mjini Cotonou, Benin na kuifanya isalie na pointi saba na sasa italazimika kushinda mechi ya mwisho ya Aprili 3 dhidi ya USGN ya Niger iliyolazimisha sare ya 2-2 nyumbani na RS Berkane ya Morocco mjini Niamey.
Simba ikishinda mchezo huo itafikisha pointi 10 na kuungana na moja kati ya Berkane au Asec zitakazovaana katika mechi ya mwisho ili kutinga robo fainali ya michuano hiyo ya Shirikisho na kuandika historia mpya.
Katika mechi ya jana Simba ilienda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 yakifungwa na Aubin Kramo dakika ya 16 na Aziz Ki dakika 25, huku kipa Aishi Manula aliokoa penalti ya Karim Konate dakika ya 36.
Manula pia aliokoa penalti nyingine ya wenyeji dakika 88 iliyopigwa Anicet Oura baada ya Onyango kufanya madhambi. Bao la tatu la Asec inayoongoza kundi hilo kwa sasa na pointi 9 lilifungwa na Konate.
Pablo alikiri michuano ni migumu kwani kila timu inashinda nyumbani, hivyo anaamini mechi ya mwisho dhidi ya USGN itawapa tiketi ya robo fainali.
“Mechi ya Aprili ndio fainali yetu, lazima tushinde.”