Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sure Boy: Ni mkali mmoja tu anayenimudu Bongo

KIUNGO fundi wa Azam FC, Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ anaamini mpira unawaheshimu mastaa watatu mpaka watano kwenye Ligi Kuu Bara na wanautendea haki kwa mtazamo wake. Lakini kwa timu pinzani ni mchezaji mmoja tu wa Mtibwa anamjulia.

Mchezaji huyo ambaye mara nyingi unapofika wakati wa usajili amekuwa akihusishwa na kujiunga na Yanga, amewataja na sababu.

Kwa kuanzia anasema akiambiwa acheze na straika gani kwenye mechi ngumu, basi atamchagua John Bocco anayecheza Simba kwa sasa, akiamini hawawezi kukosa ushindi.

“Bocco analijua goli, nimecheza naye kwa muda mrefu, najua namna anavyojua kupambana na ndio mchezaji anayeongoza kwa mabao mengi kwa kizazi cha sasa hizo rekodi zipo wazi,” anasema.

Anasema kwa wageni straika wa zamani wa Azam FC, Kipre Tcheche atabaki kuwa bora kwa uwezo na upambanaji wake ambao uligeuka funzo kwa wazawa na aliwatendea haki mashabiki kupata burudani.

Anamtaja Clatous Chama wa Simba, kwamba hakuna mchezaji ambaye hatapenda kucheza naye katika mechi ngumu na zenye ushindani akitaja sifa zake kwamba ni tajiri wa madini katika miguu yake. “Chama ni fundi anayependa soka lazima utatamani kucheza naye, si mchezaji mwenye mabavu ila akili yake inawafanya mabeki wacheze rafu na timu yake kupata faida ya kufunga mabao,” anasema.

Nje na Chama, anasema Papy Tshishimbi anamvutia namna ambavyo anajua kutumia kipaji chake, mnyumbulifu na anasambaza mipira pale kati, huku akiwa na uwezo wa kufunga na kukaba.

Kwa upande wa Haruna Niyonzima, anasema ni mfano tosha wa kuigwa na wachezaji wazawa na wageni jinsi ambavyo anajitunza na soka linamheshimu, akisisitiza kwamba kwa muda wote ambao amecheza Tanzania thamani yake bado kubwa.

“Amekuwa akicheza kwenye kiwango cha juu, hachuji wala hachukizi, akicheza unaona burudani ya aina yake hao ndio aina ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kuleta afya ya soka letu na sio wanakuja wanaanza kusota.”

KISIGA NA AWADHI

Anasema wakati anachipukia kwenye soka alikuwa anamtazama Shaban Kisiga (alicheza Simba sasa yuko Ruvu Shooting) kama mfano wa kuigwa, anakiri ni kati ya vipaji vilivyomshangaza na vinaendelea kumshangaza anapomuona uwanjani.

“Kisiga alikuwa akicheza basi nilikuwa naacha kila kitu kwenda kumtazama, fundi, nidhamu mbele, mbinu, kifupi amekamilika kila kitu na tunapaswa kujifunza kitu kutoka kwake kwani bado ana uwezo wa kucheza popote kuliko chipukizi,” anasema.

Anamtaja kiraka Awadhi Juma wa Mtibwa Sugar kwamba wakikutana kwenye mechi ndiye anayemsumbua kiasi kwamba wanatoana jasho kwa aina ya uchezaji. Anakiri ndiye mchezaji pekee anayemmudu zaidi Bongo.

“Jamaa ni kama ananijulia, tukienda kucheza na Mtibwa Sugar lazima niumize akili jinsi ya kufanya kazi zangu kwa ufasaha mbele yake, naamini hata yeye anapata shida na mimi, kifupi pale kati panakuwa pamoto.”

VIJANA HAWAHESHIMU WAKONGWE

“Tuliwekewa misingi na wazee wetu, kaka zetu nyakati zao zimepita hivyo na sisi hatuwezi kudumu milele lazima tuanze kuheshimu wengine na sisi tutaheshimiwa baadaye, ila tukileta ujuaji tutapotea kirahisi na rekodi za wakongwe zitaendelea kudumu,” anasema.

KUTUNZA KIWANGO CHAKE

“Naheshimu walionitangulia, napenda kujifunza, msikivu wa kuyafanyia kazi yale yanayokuwa yanaelekezwa kwetu na wadau mbalimbali wa soka kwani wengi wao wameacha rekodi nzito wakati wanacheza soka hivyo wanajua wanachokisema.

“Sina starehe nyingine zaidi ya soka, sivuti bangi wala sigara, sinywi pombe wala kwenda disko, nina muda wa kukaa na washikaji kubadilishana mawazo hapa na pale kisha kuendelea na mishe zangu zinazonipa kipato,” anasema mchezaji huyo na kuongeza kuwa baba yake, Aboubakar ambaye alicheza kwa mafanikio Yanga amekuwa akimpa changamoto za jinsi za kupambana kufikia malengo.

Anasema watu waliopo nyuma yake wanaounga mkono juhudi zake ni baba yake mzazi na Herry Mzozo, ambao wanafuatilia kila anachokifanya akiwa kwenye ubora na kushuka kiwango.

“Mzee huwa ananiambia una kazi ya kupambana mpaka kupiku kile nilichokifanya kwenye Ligi Kuu, hivyo ananipa mtihani wa kufikia na kupitiliza.

“Anasema ni kweli napambana ila nisijione nimefika nikae nikijua kuna watu walifanya makubwa, wameweka alama hivyo anataka niweke alama ya kwangu na nisikubali kutundika daruga kizembe.”

Anasema katika historia yake ya soka hataacha kuliimba jina la kiongozi wa Friends Rangers, Herry Mzozo ambaye amemshika mkono mpaka anajulikana kila sehemu.

“Ni baba yangu wa soka, mshauri wangu kwa ujumla, ana mchango mkubwa wa mafanikio yangu, anakusaidia bila kutaka kitu, anapenda kukuona unafika mbali hiyo ndio maana sahihi ya mtu wa soka.

“Ananifanya niwe najituma kwa bidii kwa sababu nikianza kushuka tu nakuwa na cha kujibu, watu wanamuona mkorofi kwa sababu hapendi vitu vya kupinda pinda.”

PESA KUBWA YA KWANZA

Sure Boy anasema wakati anacheza Friends Rangers, kuna timu ya Zanzibar ilikuwa inaitwa TZDL ya daraja la pili, ilikuwa inawakodisha kushiriki katika mashindano mbalimbali.

“Nakumbuka sikuwepo katika chaguo la kwenda Zanzibar, lakini wakati wanacheza mechi ya mwisho siku hiyo nilicheza nikaonyesha kiwango cha juu, yule kiongozi wa timu hiyo akanichagua nijiunge na wengine,” anasema na kuongeza:

“Nikaenda huku timu ikachukua ubingwa, tukapewa Sh70,000, nikanunua redio kubwa hivyo nikawa na muziki mnene getho, nikamwambia Mzozo alicheka sana akasema una akili ya kufikiria kesho.”

TAIFA STARS IFANYE HIKI

Sure Boy ni kati ya wachezaji walio muhimili kwenye kikosi cha Taifa Stars ameona jambo na kulishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba linahitaji uwekezaji wa muda mrefu wa kizazi kitakachokuja kufanya maajabu.

Anasema wanahitajika kuandaliwa wachezaji ambao wataleta mapinduzi ya kufanya maajabu katika michuano ya kimataifa na sio kwa staili wanayokwenda nayo kwa sasa.

“Nilikuwa najutia sana kwani kuna wakati nilikuwa naona wazi kwamba nakosa mechi wakati nahitajika, ujue zinakuwa ni hasira za kwenye soka tu ndani ya dakika 90 tukijaribu kupambania ushindi.”

ANALIDAI SOKA

Anasema anaendelea kulidai soka ingawa limemlipa kwa sehemu, kwamba anaamini akiendelea kupambana atapata kile anachokitarajia.

“Bado nina muda wa kupambana kuhakikisha kipaji changu kinanilipa kama ninavyotaka, inawezekana kwa sharti la kukaza msuli,” anasema huku akiongeza kuwa ana mipango ya kucheza nje ya nchi na sasa anajipanga.

AZAM INAKWAMA WAPI UBINGWA?

“Kuna changamoto za ratiba, waamuzi, hivyo tunajikuta tukipambana kila wakati, ila ipo siku tutakuja kupindua meza dhidi ya Simba na Yanga ambazo zinapokezana kwa sasa.”

NI FUNDI MAGARI

Anasema kama sio soka angefanya kazi ya ufundi wa magari kwa sababu ameisomea.

“Nimesomea ufundi magari ninajua kutengeneza magari ndio kazi ningefanya kama isingekuwa soka,” anasema.

MACHUNGU YENYE ALAMA MOYONI

Anasema mwaka 2018 wakiwa kwenye Kombe la Mapinduzi, Zanzibar mama yake mzazi alifariki dunia, jambo ambalo lilimuumiza kupita kiasi.

“Nilimuacha mama anaumwa Dar es Salaam, nikaenda Zanzibar, nakumbuka siku hiyo nililala ndani sasa nikawa naenda chooni, chumbani nilikuwa na Himid Mao,” anasema na kuongeza:

“Philipo Alando kipindi hicho alikuwa meneja, akawa anaongea na Himid huku ananiangalia, nikajibanza mlangoni kujua wanaongea nini, ndipo nikasikia wakiongea habari za mama yangu, aisee nililia sana.”

UCHAWI NDONDO

Anasema siku moja walikwenda kucheza akiwa na timu yake ya Zaragoza ya Magomeni na timu moja ya Mburahati, kilichotokea bado anajiuliza mpaka leo.

“Mimi na mwenzangu tulichelewa kufika uwanjani, nikawa mbele mbele kuingia nikakumbuka nimesahau kuvaa soksi, nirudi nyuma mwenzangu akakutwa na masaibu,” anasema.

“Akawa analia haoni, basi wakajaa watu kumwangalia likawa tukio la kusikitisha mechi ikavunjwa, ilitubidi kwenda naye kwa shehe akamuombea ndipo akaona tena.”

MECHI KALI

Sure Boy anasema hatausahau msimu wa 2013/14 ambapo Azam FC ilitoka sare ya mabao 3-3 na Mbeya City katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akisimulia jinsi mechi hiyo ilivyokuwa ngumu, anasema Mbeya City ilikuwa na ushindani wa hali ya juu na ndani ya kikosi chao walikuwemo kina Deus Kaseke, Peter Mwalyanzi na wengine.

“Hiyo ni mechi ambayo sitakaa niisahau kwani baada ya dakika 90 wachezaji wa Azam FC hatukuwa na raha kufungwa nyumbani, ile Mbeya City ilikuwa moto kwa kila timu,” anasema.

MAKOCHA BORA

Anasema Azam FC wamepita makocha wengi, lakini ambao anawakubali ni Aristica Cioba na Stewart Hall.

Anasema: “Nakumbuka kipindi cha Hall timu ilikuwa moto hata kipindi cha Cioaba ni zaidi ya makocha wanatufanya tuwe kitu kimoja na tupambane.”

“Ni makocha ambao wanataka tukae profeshno zaidi, wanataka tufikirie mbali zaidi na tuishi kama wanasoka wa Ulaya.”

KIKOSI CHAKE HIKI HAPA

Sure Boy anacho kikosi bora ambacho yeye anajiweka eneo la ukocha huku kipa wake akiwa ni Mwadini Ally, Shomary Kapombe, Bruce Kangwa, Agrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Clatous Chama, Haruna Niyonzima, John Bocco, Mudathir Yahya na Shaban Kisiga.