Straika Mserbia gumzo Simba

Straika Mserbia gumzo tupu Simba

MASHABIKI wa Simba juzi Jumamosi usiku walitoka Uwanja wa Benjamin Mkapa vichwa chini baada ya timu yao kupasuliwa mabao 2-1 na Yanga, huku wakisonya wakimtupia lawama Kocha Zoran Maki kwa kumchezesha Dejan Georgijevic katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii na kushindwa kung’ara.

Straika huyo kutoka Serbia, aliingizwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Habib Kyombo, jambo lililowaibua nyota wa zamani wa klabu hiyo waliomkosoa, licha ya kocha mmoja maarufu kumtetea na mashabiki kumgeuza kuwa mjadala mitaani na mitandaoni.

Dejan aliyesajiliwa na msimu huu wa dirisha kubwa ameibua mijadala hiyo baada ya kuonyesha kiwango hafifu kwenye mchezo huo, huku Fiston Mayele akifunga mara mbili kupindua meza baada ya awali Pape Ousmane Pape kuitanguliza Simba kwa bao la kipindi cha kwanza.

Baadhi ya nyota wa zamani wa Simba waligawanyika juu ya mchezaji huyo, huku wengi wakimponda na kusema ni mchezaji wa kawaida sana.

“Binafsi namuona ni mchezaji wa kawaida kabisa, hata Mpole (George) anamzidi,” alisema kiungo fundi wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mtemi Ramadhani.

Mtemi alisema Dejan anaweza kuwa mchezaji mzuri huko alikotoka, lakini kwa soka la Tanzania ni wa kiwango cha kawaida kuweza kuisaidia Simba.

“Hata Mpole anaweza kuwa zaidi yake, labda kwenye mechi za kimataifa anaweza kuisaidia timu, lakini kwenye ligi yetu hapana, akutane na mabeki kama Nyoso au Yondani ndio kabisa,” alisisitiza Mtemi, kauli iliyofanana na ile iliyotolewa na nyota wa zamani wa Simba, Malota Soma.

Malota alisema anamuona Dejan kuwa mzito na kwa soka la Kiafrika itamchukua muda kumudu na kuonyesha kiwango ambacho mashabiki na wapenzi watamuamini.

“Labda tumpe muda, lakini wenzetu hawa mechi za Kiafrika huwa ni vigumu sana kuzimudu, sisi tunacheza mtu na mtu, wao wanacheza kwa nafasi, labda tumpe muda ili azoee soka letu,” alisema.

Hata hivyo, Kocha Abdul Mingange amemtetea mchezaji huyo akifichua kwamba ana kiwango kizuri zaidi hata ya Kyombo kwenye kikosi cha Simba.

“Bado hajajuliwa jinsi ya kumpa mpira, tatizo soka la Tanzania tunapenda sana ile anao anao, hivyo hadi wanampa pasi Dejan anakuwa tayari kwenye offside, lakini ni mchezaji mzuri wakijua namna ya kumchezesha, ni zaidi ya Kyombo,” alisema.