Sopu aanika siri ya hat-trick yake

Sopu atwaa kiatu cha ufungaji bora ASFC

MABAO matatu 'hat-trick' aliyofunga Abdul Suleiman ‘Sopu’ katika fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga juzi, yamemfanya mshambuliaji huyo wa Coastal Union kuwa kitovu cha vita ya mabosi wa Simba na Yanga wanaoitaka saini yake huku wakiivamia kimafia Azam iliyotangulia kuzungumza naye.

Sopu alifunga ‘perfect hat trick’, kwa kutumia kichwa na miguu yote miwili wakati Coastal ikifa kwa penalti 4-1 mbely ya Vijana wa Jangwani baada ya sare ya 3-3 katika dakika 120 za mchezo huo wa fainali kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Inaelezwa kiwango alichokionyesha Sopu katika mchezo huo, kiliwashtua mabosi wa klabu hizo kubwa na kumtwangia simu kwa nyakati tofauti, jambo lililothibitishwa na mchezaji mwenyewe pamoja na uongozi wa Coastal ambao uliitaja Azam kwamba ndiyo iliyoanza mapema kumvizia.

Inaelezwa baada ya mechi ya juzi kumalizika, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said akiwa na mabosi wengine wenye nafasi ya uamuzi usiku usiku walimfuata Sopu na kuzungumza naye kimyakimya, wakionyesha nia ya kuitaka saini yake.

Mabosi hao wa Yanga, walimueleza Sopu wamevutiwa na kiwango chake si katika mechi hiyo ya fainali bali alichoonyesha kwenye ligi na mashindano mengine msimu huu mzima na uliopita ambao alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi.

Baada ya mazungumzo hayo yenye usiri mkubwa Sopu akiwa anawasiliana na wasimamizi wake alieleza maslahi ambayo anayahitaji na Yanga kama itakuwa tayari kumpatia atamwaga wino wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Mara baada ya kumalizana na kina Hersi, inaelezwa Sopu alipokea simu nyingine kutoka kwa bosi mmoja wa juu wa Simba aliyemueleza wapo tayari kumaliza mazungumzo waliyofanya mara ya kwanza ambayo hayakufikia mwisho kwa vile timu hiyo ilikuwa haina kocha mkuu.

“Tumeongea na Sopu mapema ila kiwango alichoonyesha kwenye mechi ya Yanga, naamini thamani yake itakuwa imeongezeka na tumueleza tupo tayari kukaa naye tena mezani kuona kama tutakubaliana ili kumrudisha Simba, kwa maslahi mazuri kwetu na kwake,” kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa juu wa Coastal (jina tunalo) aliliambia Mwanaspoti kuwa, Yanga waliwapigia simu na kuwajibu kwamba kama wanamtaka Sopu ni lazima wakubaliane na Azam kwani klabu hiyo ilikuwa ya kwanza kumfuata na ilikamilisha asimilia 90 ya mazungumzo.

Kigogo huyo alisema Azam imekubaliana na mchezaji na klabu ya Coastal kutoa kiasi cha pesa kama thamani ya mkataba uliobaki wa Sopu au udhamini ili kupata huduma ya mchezaji huyo msimu ujao awepo kwenye viunga vya Azam Complex.

Inaelezwa kuwa, Sopu muda wowote kuanzia leo Jumatatu atakutana na mabosi wa Azam wakiongozwa na mmiliki, Yusuf Bakhresa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’ kama watakubaliana watakamilisha dili hilo.

Kupitia kwenye mtandao wa Instagram, Yusuf aliombwa na mmoja wa mashabiki wa timu hiyo kumsajili Sopu na alijibu kwa kifupi “Usiwe na wasiwasi. Tutulie.”


MSIKIE SOPU

Mwanaspoti ilimtafuta Sopu, ambaye alikiri kupigiwa simu usiku na vigogo wa klabu hizo kubwa nchini, akifafanua pia Azam walishazungumza naye mapema, lakini hajafanya uamuzi.

Sopu alisema bado ana mkataba wa miaka miwili na Coastal kwa maana hiyo timu hizo zote amezieleza ziwasiliane kwanza na uongozi wake kisha wakikubaliana ndio wamfuate.

Naye Mwenyekiti wa Coastal, Steven Mnguto alisema baada ya msimu huu Sopu atakuwa amebakisha mkataba wa miaka miwili, hivyo Simba, Yanga na Azam wote wameelezwa kulipa gharama ya kuununua mkataba huo.