Namungo FC yamrejesha Kikoti

Muktasari:
- Kikoti alijiunga na Coastal Union msimu wa 2023/24 akitokea Namungo na kudumu hadi 2024/25.
MABOSI wa Namungo wameamua kumrejesha nyumbani kiungo mnyumbulifu, Lucas Kikoti ambaye msimu uliopita alikuwa akicheza Coastal Union.
Kikoti alijiunga na Coastal Union msimu wa 2023/24 akitokea Namungo na kudumu hadi 2024/25.
Mwanaspoti linafahamu mchezaji huyo amejiunga na Namungo kwa mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Ruangwa mkoani Lindi kwa kuanzia msimu ujao.
Nje ya Kikoti, Namungo pia imemsajili mshambuliaji, Abdulaziz Shehame aliyekuwa na klabu ya TMA inayoshiriki Ligi ya Championship.
Shehame msimu uliopita akiwa na klabu hiyo, aliifungia mabao 18 akiwa miongoni mwa wafungaji bora sambamba na Raizin Hafidh (Mtibwa Sugar) na Andrew Simchimba (Geita Gold).
Nyota mwingine aliyejiunga na Namungo ni Kiraka, Cyprian Kipenye ambaye alikuwa anacheza kwenye kikosi cha Songea United na hivi karibuni alikuwa kwenye majaribio katika klabu ya Simba inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Chanzo kutoka ndani ya Namungo kililidokeza Mwanaspoti kwamba usajili huo ni lengo la kuendelea kuboresha kikosi chao. “Hawa wote ni wachezaji wazuri, tutaendelea kufanya usajili kwa sababu tupo kwenye mazungumzo na nyota wengine na lengo ni kuisuka timu yetu,” kilisema chanzo.