Sakho, Inonga kupangua kikosi Simba

Mshambuliaji wa Simba, Pape Sakho.

Dar es Salaam. Kupona kwa mshambuliaji wa Simba, Pape Sakho na uwepo wa beki mkongomani Hennock Inonga huenda kukaleta mabadiliko katika kikosi cha cha kwanza cha Simba chini ya kocha Pablo Franco.

Hiyo ni kutokana na ubora wanaouonesha wawili hao mazoezini, huku kila mmoja akiwa bora kwenye eneo lake na tayari kocha Pablo ameanza kuwaweka kwenye mipango yake kuelekea mechi ya

Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, kesho.

Katika mazoezi ya juzi ya Simba yaliyofanyika Uwanja wa Mo Simba Arena Bunju, Sakho na Varane walikuwa panga pangua katika kila programu, huku wakionesha ubora mkubwa wa kuanzisha mashabulizi, kukaba, kuziba nafasi na kuupanga ukuta kwa upande wa Inonga huku Sakho akiteka uwanja kwa chenga, spidi, pasi na mashuti mazito ambayo mengi yalizaa mabao.

Wawili hao walisajiliwa na Simba msimu huu na kabla ya ujio wa kocha Pablo hawakuwa na nafasi ya kuaminika ndani ya kikosi hicho chini ya kocha Didier Gomes aliyeachana na timu hiyo kwa makubaliano maalumu mapema mwezi huu.

Katika kikosi kilichokuwa pamoja kwa muda mrefu katika mazoezi ya juzi, Pablo aliwapanga Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Husasein, Joash Onyango, Inonga, Jonas Mkude, Rally Bwalya, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Sakho na Benard Morrison ambao walicheza kwa maelewano makubwa.

Kama wawili hao watapenya na kuingia katika kikosi cha kwanza, Inonga atakauwa amechukua nafasi ya Pascal Wawa au Kennedy Juma ambao wamekuwa wakicheza kwa kupokezana katika michezo iliyopita na Sakho atachukua nafasi ya Kibu Denis na Hassan Dilunga.