Sakho achimba mkwara mzito Simba

Friday August 05 2022
sakho pic
By Thobias Sebastian

MFUNGAJI wa bao bora katika mashindano ya kimataifa msimu uliopita kwenye ngazi ya klabu, Pape Ousmane Sakho amesema moto aliomaliza nao msimu huo huo ndio ataanza nao.

Sakho alisema wakati anafika Simba hakuwa na mwanzo mzuri kutokana na changamoto mbalimbali za kupata nafasi ya kucheza pamoja na majeraha ya mguu aliyopata mwanzoni kabisa.

Alisema katikati ya msimu hadi mwisho alikuwa fiti na kuzoea kucheza mashindano ya ndani na ya kimataifa huku akionyesha kiwango bora lilikuwa jambo kubwa kwake.

“Kutokana na maandalizi ambayo nimefanya huku Misri na wachezaji wenzangu pamoja na kiwango nilichoonyesha katika mechi za mwisho za msimu uliopita kwenye mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika, natarajia kuwa bora zaidi msimu huu, nataka kuanza nilipoishia,” alisema Sakho na kuongeza;

“Kiwango nilichoonyesha katika mashindano ya kimataifa ilikuwa faida kwa timu pamoja na upande wangu hadi kupata moja ya tuzo kubwa hapa Afrika katika mashindano hayo makubwa zaidi kwenye ngazi ya klabu.

“Sitamani kuona naanzia chini. Nikifanikiwa kuonyesha kiwango bora nitaisaidia timu kufanya vizuri kwenye mashindano yote kwa hiyo mashabiki wetu watulie na wanatakiwa kuwa pamoja nasi katika nyakati zote.

Advertisement

“Simba imeongeza wachezaji wengine bora kwenye kikosi chetu haswa wanaocheza nafasi za mbele, kwa maana hiyo natakiwa kuwa bora.”

Sakho alisema timu yao imekuwa na ushindani mkubwa ndani ya kikosi na itakwenda kuwa hivyo hadi kwenye mechi za kimashindano na lengo kubwa ni kufuta zile rekodi mbaya za msimu uliopita ambazo hakuna hata mchezaji mmoja anapendezewa nazo.

Msimu uliopita Sakho alishinda tuzo moja ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu na pia kuchaguliwa kwenye kikosi cha wachezaji 11 bora wa Ligui Kuu Bara katika tuzo za msimu za TFF.

Advertisement