Rayan, Laman watua Hispania kunoa kucha

WACHEZAJI wawili wa Kitanzania, Rayan Ramadhani na Laman Sadik Kaunda wametua Hispania kwa ajili ya kujiunga na akademi ya RUSH-SPF iliyopo Valencia kwa ajili ya programu maalum zenye lengo la kuimarisha vipaji vyao.
Kwa mujibu wa Seif Mpanda ambaye vijana wake wapo kwenye akademi hiyo, Jabir na Tariq alisema uhusiano wa karibu baina yake na akademi hiyo umesaidia Rayan na Laman kupata nafasi ya kwenda Hispania kujifunza mambo mbalimbali.
“Kuna kila uwezekano kuwa huenda wakajiunga na kituo hicho moja kwa moja kama ilivyo kwa vijana wangu, Jabir na Tariq. Nimekuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na wazazi wa Rayan na Laman hivyo ilikuwa rahisi kusaidia vijana hao kupata nafasi.
“Nadhani Rayan na Laman wamehamasika baada ya kuona marafiki zao ambao ndio vijana wangu wakiwa Hispania, nilivyoelezwa kuwa nao wanataka kwenda huko, baada ya wazazi wao kukubali, tukafanikisha hilo kwa pamoja,” alisema.
Rayan na Laman wameonekana kufurahia kutua kwao Hispania ambako wataungana na wachezaji wenzao wa Kitanzania ambao ni marafiki zao wa karibu, Tariq na Jabir kwa ajili ya kupigania ndoto zao za kuwa wachezaji wakubwa kwa miaka ya baadaye.
Wakati wakiwa Tanzania, Rayan na Laman walikuwa na programu maalum za mazoezi chini ya kocha Mjerumani, Martin Hammel ambaye pia huwa anamnoa Barka Seif.