Prisons yakusanya tatu nyingine kwa Wagosi wakaya

Muktasari:
- Matokeo hayo yanakuwa na nafuu kwa Tanzania Prisons ambayo ilikuwa na mwanzo mgumu kwenye Ligi Kuu ya NBC.
Mbeya. Mdogo mdogo. Ndivyo unaweza kusema baada ya leo tena Tanzania Prisons kuondoka na alama tatu muhimu kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Sokoine jiji hapa.
Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Wajelajela hao baada ya mechi iliyopita kuifunga Dodoma Jiji mabao 3-2 na kuendelea kuvuta matumaini ya kukwepa kushuka daraja.
Katika mchezo huo, Prisons walionesha kasi wakishambulia zaidi na kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya saba kupitia kwa Oscar Paul na kufanya kwenda mapumziko wakiwa mbele dhidi ya Wagosi wa Kaya.
Hata hivyo Coastal Union walijipapatua kutaka kusawazisha lakini walikutana na upinzani dhidi ya wapinzani hao ambao ndio walikuwa wenyeji katika uwanja huo wa Sokoine.
Kipa wa Coastal, Mussa Mbisa alishindwa kuendelea na mechi baada ya kuumia wakati akipambana kuokoa moja ya shuti lililokuwa likielekea langoni mwake na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Mohamad katika dakika ya 31.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ambapo Prisons walimtoa mfungaji wa bao, Paul, Ezekiel Mwashilindi, Athanas Mdamu na Nurdin Chona na nafasi zao kuzibwa na Benjamin Asukile, Mohamed Mkopi, Aboubakari Malika na Ramadhan Ntobi.
Kwa upande wa Coastal walimtoa Vincent Aboubakari na Benedict Jacob na kuwaingiza Haji Ugando na William Kisingi katika dakika tofauti.
Pamoja na mabadiliko hayo kutobadili matokeo, lakini timu zote zitajilaumu kwa kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata japokuwa Kipa wa Prisons Hussein Abel alikuwa imara langoni kwa kuokoa hatari.
Kwa matokeo hayo, yanaifanya Prisons kufikisha alama 19 lakini ikibaki nafasi yake ya 15 huku Coastal Union wakibaki na alama zao 21 katika nafasi ya 14.