Ninja aibuka na faili la Miquissone

Tuesday May 04 2021
ninja pic
By Khatimu Naheka

YANGA imeingia kambini tayari kuanza maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Simba utakaopigwa Mei 8, lakini beki wao mmoja aliyekatika mzuka mkubwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amefungua mdomo wake kuelekea mchezo huo akiibua faili la staa wa wekundu hao, Luis Miquissone.

Akizungumza na Mwanaspoti juzi, Ninja alisema anawajua na ameshawahi kukutana na washambuliaji wote wa Simba, lakini faili analopambana kulisoma kwa umakini ni lile la Luis Miquissone pekee ambaye hajawahi kukutana naye.

Ninja alisema anawaheshimu Simba na kwamba ina wachezaji wazuri lakini hata wao kila beki ana hamu ya kukutana na wekundu hao kisha wamalizane.

Beki huyo asiyejua kuremba alisema mchezo huo hautakuwa rahisi na kwamba hesabu zake sasa ni jinsi ya kukabiliana na Luis ambaye anafahamu kwamba si mshambuliaji mchezo-mchezo.

“Washambuliaji wote wa Simba nimewahi kukutana nao wala sina wasiwasi nao, kikubwa nawapa heshima tu kwa kuwa nao ni wazuri ila siwezi kuogopa lolote tukikutana wanajua hilo,” alisema Ninja.

“Pale Simba mtu ambaye sijawahi kukutana naye ni Miquissone tu lakini naye tayari najua jinsi gani ya kuweza kukabiliana naye, ni mchezaji mzuri ila hutakiwi kumpa nafasi ya kufanya uamuzi anaweza kuleta madhara.

Advertisement

“Hao wengine ni kwamba kila hatua unatakiwa kuanza kuamua wewe kabla ya wao hawajaamua na hilo hata kocha wetu (Nesreddine Nabi) amekuwa akitusisitizia kwamba ni makosa beki kuacha mshambuliaji afanye uamuzi kabla yako na hili sio gumu kwangu na naamini hata kwa wenzangu,” alisema akiongeza anafurahia kuanza kuelewa kipi Nabi anataka kifanyike.

Advertisement