Nabi: Kuna mshtuko unakuja

Sunday November 14 2021
NABI PIC
By Thobias Sebastian

YANGA inarejea Dar es Salaam leo kutokea kambini Zanzibar tayari kwa mkao wa kwenda Mtwara kuwakabili Namungo kwenye mechi ngumu ya Ligi Jumamosi ijayo.

Kocha Mkuu, Nesreddine Nabi amesisitiza kwamba kwa ushindani aliouona kambini, anaamini ligi ikiendelea wachezaji wake wakiendeleza kujituma watashtua watu wengi kwani wameiva.

Anasema kwamba hata walioko kwenye timu za Taifa wakirejea ushindani utakuwa mkubwa kwani kuna kitu amekiona kwa hawa aliokuwa nao kambini Unguja.

Alisema katika kambi hiyo wamepata nafasi ya kufanya mazoezi mengi ya mbinu na nguvu ikiwemo na kucheza mechi mbili za kirafiki na kila mchezaji ameonyesha nia ya kutaka kupewa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

“Nimefurahishwa na wachezaji waliokuwa katika kambi hii kwani wamepambana kwa kuonyesha wanastahili kupewa nafasi ya kucheza katika mechi za ushindani hili ni jambo jema kwetu,” alisema Nabi ambaye ana uraia wa Tunisia na Ubeligiji.

“Jambo hilo litaongeza ushindani katika timu lakini hakutakuwa na tofauti kubwa kati ya wale ambao wanapata nafasi ya kuanza na watakaokuwa benchi kila ambaye atapata nafasi atafanya kazi yake ipasavyo. ”

Advertisement


KUHUSU YACOUBA

Nabi alisema kuumia kwa Yacouba Sogne si kitu kizuri kama timu kwani ni miongoni mwa wachezaji ambao walianza msimu vizuri.

“Hata tukifanya mabadiliko ya mchezaji katika nafasi hiyo hatutaondoka katika mfumo wetu, ambao tumeanza nao vizuri kwa kila mchezaji kutimiza majukumu yake na kupata matokeo ya ushindi katika mechi tano za ligi,” alisema Nabi.

Kukosekana kwa Yacouba kutokana na majeraha ya goti, nafasi ya winga ambayo alikuwa akicheza anaweza kuanza mmoja kati ya hawa watatu, Farid Mussa, Deus Kaseke, Rajabu Athumani na Dickson Ambundo ambaye hajacheza mechi yoyote ya ligi msimu huu tangu alivyosajiliwa kutokea Dodoma Jiji. Yanga inapambana kufanya vizuri msimu huu ili kurejea kwenye ramani ya makombe ambayo yaliadimika Jangwani kwenye miaka ya hivikaribuni. Tayari wameshabeba ngao ya hisani kwa kuwafunga Simba bao 1-0 Jijini Dar es Salaam likipachikwa na Mkongomani, Fiston Mayele ambaye ni miongoni mwa sajili mpya.

Advertisement