Nabi ashtukia mtego, awaonya wachezaji, viongozi

KOCHA wa Yanga, Nesredine Nabi ameshtukia mtego mbele yake kuelekea mechi ya watani wa jadi, Desemba 11.

Nabi ambaye timu yake imekuwa kwenye fomu katika wiki za karibuni, jana aliipeleka timu hiyo kambini mjini Unguja kujipanga upya.

Kocha huyo baada ya kuangalia mechi ya Simba na Namungo ameshtuka na kuamua kupanga upya karata kwenye mambo mawili na amekuwa na vikao vya mara kwa mara kati yake na wachezaji na viongozi kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake.

Jambo la kwanza ni dhidi ya Namungo, Mbeya Kwanza ugenini na pili Simba kwenye Uwanja wa Mkapa.

Kocha huyo wa zamani wa El Merrikh ya Sudan, ameliambia Mwanaspoti kuwa mechi hizo zimebeba umuhimu mkubwa kwenye heshima ya msimu huu katika mbio za ubingwa, utani wa jadi pamoja na rekodi.

Nabi ambaye aliyekalia kuti kavu mwanzoni mwa msimu huu, alikuwa uwanjani siku chache zilizopita wakati Namungo ikikubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya Simba kwenye Uwanja wa Mkapa.

Ameliambia Mwanaspoti kuwa Namungo sio timu rahisi na kuna vitu wanapaswa kuvifanyia kazi kwa haraka sana.

Nabi ameweka wazi pia kikosi chake kitakuwa na ratiba ngumu ya mtego kwani baada ya Namungo watawafuata Mbeya Kwanza Novemba 30, kabla ya kurudi Dar kuwavaa Simba Desemba 11 mechi waliyoiwekea uzito mkubwa, kisha watawafuata Prisons Desemba 19.

“Utaona hiyo ni ratiba ngumu ambayo tunahitajika kuwa na maandalizi maalumu ya kuwa fiti ili tuweze kukabiliana nayo tuweze kufikia malengo yetu ya msimu huu,” alisema Nabi mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji.

“Tumewaona Namungo ni timu ngumu inatumia nguvu sana na nafahamu watakapokuwa nyumbani watakuwa wagumu zaidi. Tu-tajipanga vizuri kukabiliana nao.Ukiachana na Namungo utaona hatuna mechi rahisi zote zinazofuata ni ngumu zinahitaji akili yetu ijiandae na ugumu huo. Kwa hiyo ipo ratiba ambayo tutaitengeneza ili tuwe sawasawa na tutaanza hapahapa wakati wa mapumziko ya ratiba ya kimataifa.”

Nabi aliahidi kwamba kikosi kikirudi uwanjani anataka kipige pasi nyingi za kwenda mbele kuliko kurudi nyuma.

Katika kuanza kuibadili Yanga, Nabi juzi aliwarudisha wachezaji wake gym na huko walijifua kwa saa tatu - ratiba ambayo ilisimamiwa na kocha wa viungo Helmy Gueldish ambaye Nabi anamuelezea kama mtu muhimu zaidi kwa sasa katika mafanikio uwanjani kwani timu imekuwa na nguvu kupambana.

Akizungumzia timu hiyo, staa wa zamani wa Yanga, Nizar Khalfan alisema timu inapaswa kutumia akili nyingi na kuchanga vizuri karata zake kama wana mipango ya ubingwa kwani ushindani ni mkubwa na watakuwa na ratiba ngumu katika mechi hizo kabla ya kuwavaa Simba.

“Ukiwaangalia Namungo wa msimu huu wamefanya usajili mzuri ambao umeleta uwiano wa kikosi chao lakini pia Mbeya Kwanza wamekuwa hatari hasa kipindi cha pili wakati Yanga imekuwa imara hasa kipindi cha kwanza,” alisema Nizar aliyewahi kuinoa Yanga kama kocha msaidizi wa Cedrick Kaze.

“Hizo mbili kwanza ni mechi ngumu, lakini kitu kigumu zaidi hizo ni mechi ambazo watakuwa wanatafuta nguvu ya kwenda kucheza mechi ya watani.”