Mnigeria asaini Simba kimafia

Monday June 20 2022
akpan pic
By Waandishi Wetu

SIKU chache tu tangu ilipomshusha mshambuliaji Moses Phiri kutoka Zanaco ya Zambia, aliyekuwa akitajwa pia kuwindwa na Yanga, mabosi wa Simba wamedaiwa kufanya umafia mwingine kwa kumsainisha usiku mnene, kiungo mkabaji Mnigeria Victor Akpan aliyekuwa akitakiwa na Azam.

Akpan anayekipiga kwa sasa Coastal Union, ni kati ya wachezaji waliowahi kuripotiwa na Mwanaspoti kuwa, wapo kwenye rada za Simba sambamba na straika, Abdul Suleiman ‘Sopu’ anaichezea pia timu hiyo ya Tanga, inadaiwa kasaini miaka miwili Msimbazi.

Habari ambazo Mwanaspoti ilinasa tangu juzi usiku ni mabosi ws Azam waliitana kwenye ofisi zao za Mzizima kuzungumza na uongozi wa Coastal akiwamo mwenyekiti, Steven Mnguto na Akpani walikubaliana kumalizana jana asubuhi, lakini inaelezwa Simba ikapindua ngoma usiku huo huo.

“Azam walikubaliana leo (jana) wakutane tena wajue wamefikia wapi juu ya mshahara, alioutaka Akpan, kumbe Simba ilijua kuna hicho kikao basi jana (juzi) hiyohiyo usiku ikamfuata Akpan na kumalizana naye,” alisema mmoja wa mabosi wa Coastal aliyeomba kuhifadhiwa jina.

“Leo sasa (jana), Azam wakimsaka Akpan ili wamalize wakaambiwa tayari alishakutana na Simba usiku wa jana (juzi) na ameshasaini kisha kusafiri kwenda Lindi kwa mchezo ujao dhidi ya Namungo.”

“Yaani usajili wa huyu jamaa ni kama filamu hivi, unajua viongozi wa Azam walikuwa na hakika ya kumnasa Mnigeria huyo, walikubaliana juu ya dau la kuvunja mkataba wake Coastal na fedha za usajili,” kilisema chanzo chetu kutoka Coastal na kuongeza;

Advertisement

Taarifa hizo zinaeleza Simba mbali na mshahara, lakini mkataba wa kiungo huyo mwenye miaka 24 umevunjwa kwa dau la Sh100 milioni, huku akiahidiwa kama akiingia kwenye kikosi cha kwanza atapata bonasi za maana, mbali na kupewa marupurupu mengine.

“Akpan aliamua kusaini Simba kwa sababu ya kuamini ni timu kubwa itakayompa nafasi kujiuza katika michuano ya kimataifa, kulinganisha na Azam, ambayo licha ya kukubaliana naye, lakini aliamua kuwaacha solemba na kusaini Msimbazi,” chanzo hicho kilisema.

Hata hivyo, mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo wanasema, Akpan atasaini akirejea kutoka Lindi kwenye mechi yao ya kesho dhidi ya Namungo, kwani ashamalizana na mabosi wa Simba.

Hakuna kiongozi wa Azam wala wa Simba aliyepatikana kuweka bayana juu ya dili hilo.


MANULA FRESHI

Wakati dili hilo likimalizika hivyo, Simba pia ikafanikiwa kumalizana na kipa wao namba moja Aishi Manula ambaye naye aliwekewa fedha ndefu ili arudi Azam FC.

Simba ilimsajili Manula akitokea Azam na mabosi wa Chamazi mapema katikati ya msimu huu walimwekea fedha ndefu kipa huyo ambayo ilimtisha kukubali kusaini haraka mkataba wa kusalia kwa wekundu hao.

Hata hivyo juzi usiku tajiri wa Simba Mohammed Dewji ‘MO’ akapitisha bajeti hiyo haraka na kumfanya Manula kukubali dili hilo la miaka miwili mipya abaki klabuni.

Advertisement