Mkude, Lwanga kazi ipo

KIWANGO alichokionyesha kiungo mkabaji wa Simba, Mganda Taddeo Lwanga dhidi ya Azam FC, kimechambuliwa na wadau wa soka kama hakiwezi kumshitua mshindani wake wa namba ndani ya kikosi hicho, Jonas Mkude kuhofia kukalishwa benchi.
Aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Amri Kiemba alisema kwa namna alivyomtazama Lwanga dhidi ya Azam FC waliotoka nayo sare ya mabao 2-2, hajaona kama ana jambo jipya litakalomuweka Mkude benchi na kwamba kocha Didier Gomes anaweza akamtumia yoyote.

Alisema Lwanga ni mzuri anapokuwa na mpira, ila inapotokea unamilikiwa na wapinzani si mrahisi wa kurejea mapema kukaba, jambo analodhani akiendelea kucheza na kufanya mazoezi yatakayompa ufiti atakuwa na mwili wenye maamuzi ya haraka.
“Kuna vitu anakuwa anatamani kuvifanya, vipo anavyovifanya na vingine anashindwa, mfano kipindi cha kwanza alicheza vizuri sana anasaidia kupeleka mashambulizi, lakini ilipofika dakika ya 60 unaona kama pumzi ama kasi inapungua anakuwa anapambana sana, ndio maana nasema ngoja tuone huko mbele itakuwaje,” alisema.
Kiemba alisema uwezo wake na Mkude hauna tofauti na yoyote anaweza akatumiwa na kocha kutokana na wao kuwa ni asili wa viungo wakabaji, tofauti na Mzamiru Yasin anayecheza kwa maelekezo.
Beki wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars, William Martin alisema Lwanga ni kiungo mkabaji mzuri, lakini anatakiwa kuongeza bidii kuhakikisha anakuwa na kitu cha kushindana na uwezo wa Mkude mwenyeji wake.
“Ana ufundi wake lakini anatakiwa kuongeza bidii zaidi kwa kufanya mazoezi yakumpa pumzi ili akicheza dakika 90 awe kwenye kiwango kile alichoanza nacho dakika 45 za kwanza, ingawa sioni kama ana utofauti na Mkude ambaye amemkuta ndani ya kikosi hicho,” alisema.
Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema Lwanga ni kiungo mbunifu anaamini akicheza mechi kama tano, Watanzania wataona mchango wake katika timu ya Simba.
“Ana akili ya mpira, naamini kadri mechi zinavyoendelea atakuwa mshindani mzuri wa Mkude, nimeanza kumuona uwezo wake akiwa na timu yao ya taifa ya Uganda, ataisaidia sana Simba,” alisema.